WIZARA YA VIWANDA YAANZISHA DAWATI LA BIASHARA.
Serikali kupitia Wizara ya
Viwanda,Biashara na Uwekezaji imeanzisha dawati la wepesi wa kufanya biashara
ambao lina jukumu la kuondoa ugumu wa kuanzisha na kuendesha biashara nchini.
Hayo yamesemwa leo Bungeni na Waziri
wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji Mhe.Charles Mwijage alipokuwa akijibu swali la
Mbunge wa Magomeni Mhe.Jamal Kassim Ali.
“Ujenzi wa Viwanda nchini unategemea
zaidi mazingira ya uwekezaji yaliyopo ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa ardhi
yenye miundombinu wezeshi,sera mbalimbali,mifumo ya kodi na mifumo ya
upatikanaji wa vibali vinavyotakiwa
kisheria ambayo ni majukumu ya Serikali”Alisema Mhe.Mwijage.
Aidha Wizara ya Viwanda,Biashara na
Uwekezaji imeweka mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara
wa kitanzania ili kuwekeza kwenye viwanda hapa nchini.
Miongoni mwa Mikakati hiyo ni Mafunzo
yanayotolewa kwa watanzania wenye nia ya kuwekeza katika viwanda juu ya kuibua
mawazo ya kibiashara,kuanzisha ,kuendesha na kusimamia biashara kupitia
SIDO,kutoa ushauri wa kitaalamu wa jinsi ya kuchagua teknolojia sahihi
inayoendana na wazo la ujenzi wa kiwanda alilonalo Mtanzania kupitia
TIRDO,TEMDO na CAMARTEC na namna ya kupata ama kukuza mtaji wa ujenzi wa viwanda
kupitia NEDF,SIDO na TIB.
Pamoja na hayo Wizara imeandaa
mwongozo kwa Mikoa,Wilaya,Kata na Vijiji kutenga maeneo ,kusimamia
sheria,kanuni,taratibu na kutoa maelekezo kwa wawekezaji.
“Watanzania wnaaotaka ama walio na
mitaji mikubwa wanaweza kuwekeza kupitia maeneo ya EPZA ambayo yametengwa
mahsusi kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa zinazouzwa nje ya nchi,Pia wanaweza
kuwasiliana na TIC kupata vivutio mbalimbali vilivyowekwa na Serikali kwa ajili
ya uwekezaji,Alisisitiza Mhe.Mwijage.
Na Daudi Manongi,MAELEZO,DODOMA.

No comments