Serikali yaanzisha mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja
Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania
(TFRA) Bw. Lazaro Kitandu akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es
salaam kuhusu mfumo mpya wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (Bulk Procurement
System). Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya
Kilimo, Mifugo na Uvuvi Bw. Richard Kasuga.
Na Fatma Salum (MAELEZO)
Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea
nchini (TFRA) imeanzisha mfumo mpya wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (Bulk
Procurement System) kutoka nje ya nchi utakaosaidia kupunguza bei na
kuhamasisha matumizi ya mbolea kwa wakulima.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar
es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Bw. Lazaro Kitandu alisema
uamuzi huo wa kuanzisha mfumo mpya umekuja baada ya Serikali kugundua kuwa kwa
muda mrefu matumizi ya mbolea hapa nchini si ya kuridhisha kutokana na bei ya
mbolea kuwa juu.
“Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na
Uvuvi kwa kushirikiana na wadau wa masuala ya mbolea imeanzisha mfumo huu baada
kupitia tafiti mbalimbali zilizofanywa na wataalam waelekezi wa ndani na nje ya
nchi na kutumia uzoefu wa taasisi nyingine zinazofanya ununuzi wa bidhaa kwa
pamoja” Alisema Kitandu.
Kitandu
alieleza kuwa katika nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara (SSA), Tanzania
ni mojawapo ya nchi zenye matumizi ya chini ya mbolea kwa kutumia kilo 19 za
virutubisho hivyo kwa hekta katika ngazi ya wakulima wadogo ambapo kiasi hicho
hakiendani na malengo ya azimio la Maputo la nchi za SADC linalotaka kufikia
angalau kilo 50 kwa hekta moja.
Alisema kuwa kwa msimu wa mwaka 2017/2018 mfumo
huo utaanza na aina mbili tu za mbolea ambazo ni mbolea ya kupandia (DAP) na mbolea ya kukuzia (UREA) na mbolea nyingine zitafuata
baadaye kadri itakavyoonekana mfumo huo kuleta manufaa kwa wakulima.
Akifafanua kuhusu faida za mfumo wa ununuzi wa
mbolea kwa pamoja, Kitandu alisema utasaidia kuimarisha utaratibu wa usambazaji
wa mbolea ambapo wadau wote watakuwa na uhakika wa upatikanaji wa mbolea kwa bei
ya ushindani.
Kwa mujibu wa Kitandu pia mfumo huo utawezesha
wafanyabiashara wadogo kukua na kushiriki katika biashara ya mbolea na
kuimarisha mtandao wa usambazaji hadi ngazi ya mkulima.
“Ununuzi
wa mbolea kwa pamoja pia utasaidia kudhibiti bei ya mbolea iwapo kutajitokeza
ongezeka lisilokuwa na sababu (soko holela) kwa kuwa bei itatangazwa kwa
kuzingatia bei halisi ya mbolea, gharama halisi za usafirishaji wa mbolea, tozo
mbalimbali na kiwango stahiki cha faida ya mfanya biashara” alibainisha
Kitandu.
Serikali
kupitia mfumo huu inatarajia matokeo chanya katika kupunguza bei ya mbolea kwa
wakulima hivyo kuongezeka kwa matumizi ya mbolea na uzalishaji wenye tija ili
kuchochea maendeleo ya uchumi wa viwanda.

No comments