Tunasema asante’ Watoto majeruhi wa Lucky Vincent wazungumza hospitalini Marekani


Mjumbe wa Baraza la Congress la Marekani, Steve King-R (aliyechuchumaa) akizungumza na mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya Lucky Vincent, Doreen Mshana anayetibiwa katika Hospitali ya Mercy iliyopo Jiji la Sioux. Steve alikwenda kuwajulia hali wanafunzi watatu wa shule hiyo walionusurika katika ajali iliyotokea wilayani Karatu mkoani Arusha na kuua wanafunzi 32, walimu wawili na dereva. Kulia ni daktari bingwa, Steve Meyer. Picha kwa hisani ya Hospitali ya Mercy. 

Marekani. Maombi ya wazazi, ndugu, jamaa na Watanzania yamekuwa ni sehemu ya mafanikio ya upasuaji waliofanyiwa watoto watatu wa Shule ya Msingi ya Lucky Vincent katika Hospitali ya Mercy, Marekani.

Maombi hayo pia yamewawezesha watoto hao kuzungumza kwa mara ya kwanza jana tangu walipopata ajali ya basi, Mei 6 mwaka huu, ambapo wenzao 32, walimu wawili na dereva walipoteza maisha

Mtandao wa Siouxland Proud.com umeandika habari za watoto hao, Wilson Tarimo, Doreen Mshana na Saidia Ismael.

“Ninachoweza kusema ni asante,” amesema Wilson.

Alipoulizwa na Mjumbe wa Baraza la Congress, Steve King anaionaje Marekani, Wilson alijibu: “Napenda kila kitu.”

Na Mama yake Wilson akaongeza, “Watu wa Marekani ni wema, asante sana, tunawapenda sana.”

Saidia alisema, “Hello Tanzania.”

Kadhalika, mmoja wa madaktari waliowafanyia operesheni watoto hao, Quentin Durward alisema walilazimika kufanya upasuaji wa viungo 17, upasuaji mkubwa wa uti wa mgongo na miguu iliyovunjika zaidi ya mara moja.

“Bila upasuaji, ilikuwa ni vigumu kutabiri kama watapona lakini sasa kuna matumaini,” alisema mtaalamu wa mishipa ya fahamu, Dk Durward.

Alisema tangu wapelekwe hospitali hapo, imekuwa ni muujiza baada ya muujiza.

Pamoja na kuendelea na matibabu kwenye wodi ya watoto ya hospitali hiyo iliyopo Iowa, majeruhi hao wataanza kupewa mazoezi ya viungo katika makazi maalumu.

Mbunge wa Singida Kaskazini, (CCM) Lazaro Nyalandu ambaye alishiriki kikamilifu kufanikisha matibabu hayo, ameandika katika ukurasa wake wa Facebook kuwa maandalizi ya kuwapeleka katika makazi maalumu yameanza.

“Lakini bado wataendelea kuwa wodini kwa ajili ya uangalizi maalumu wa madaktari bingwa.” ameandika Nyalandu.

No comments