Watoto 94,000 wafikiwa na kampeni ya chanjo ya polio Gaza Kaskazini: UN

Watoto 94,000 wafikiwa na kampeni ya chanjo ya polio Gaza Kaskazini: UN
Kampeni ya chanjo ya polio ilianza Gaza mnamo Septemba 2024.
© UNRWA
Kampeni ya chanjo ya polio ilianza Gaza mnamo Septemba 2024.
4 Novemba 2024 Afya

Kampeni ya chanjo ya polio inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imehitimishwa leo eneo linalozingirwa la kaskazini mwa Gaza huku mashirika ya Umoja wa Mataifa yakiwachanja watoto 94,000, ingawa maelfu bado hawajafikiwa.

Richard Peeperkorn kutoka Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa  Duniani WHO, katika eneo linalokaliwa la Palestina amesema lengo ni kuwafikia watoto wote wa eneo la kaskazini mwa Gaza kwa dozi ya pili na ya mwisho ya chanjo hiyo.

Hata hivyo amesema vita vinavyoendelea vya mwaka mzima, wiki za kuzingirwa na amri za mara kwa mara za Israel za kuwataka watu kuhama makazi yao na mashambulizi ya mabomu vimeleta ucheleweshaji mkubwa na vikwazo katika zoezi hilo”.

Karibu asilimia 80 ya watoto wamechanjwa

Hata hivyo, shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, limesema asilimia 79 ya watoto katika Ukanda wa Kaskazini wa Gaza sasa wamechanjwa kikamilifu dhidi ya polio.

"Kusitishwa kwa mapigano kwa ajili ya misaada ya kibinadamu ni muhimu kwa kuanzishwa kwa kampeni hii muhimu, lakini bila usitishaji wa mapgano wa kudumu watoto wataendelea kuteseka na kufa," limesema shirika hio la UNRWA kwenye mtandao wake wa kijamii wa X leo Jumatatu.

Maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa walisikitishwa na matukio ya vurugu yaliyoripotiwa katika baadhi ya maeneo ambapo wazazi, watoto wao na wahudumu wa kutoa misaada walikusanyika kwa ajili ya kampeni hiyo.

Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus alielezea wasiwasi wake mwishoni mwa juma kuhusu ripoti za mashambulizi kwenye kituo cha afya.

Msichana mdogo ambaye alipoteza wazazi wake na ndugu zake katika mgomo wa kombora kwenye nyumba yao anajifunza kutembea tena kufuatia kukatwa mguu wake.
© UNICEF/Abdulrahman Subieh
 
Msichana mdogo ambaye alipoteza wazazi wake na ndugu zake katika mgomo wa kombora kwenye nyumba yao anajifunza kutembea tena kufuatia kukatwa mguu wake.

UNICEF imeitaka Israel kufanya uchunguzi

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, Catherine Russell, katika taarifa yake iliyotolewa mwishoni mwa Jumamosi, alisisitiza kwamba mashambulizi dhidi ya raia, ikiwa ni pamoja na wahudumu wa kibinadamu na kile kilichosalia cha vituo vya kiraia na miundombinu ya Gaza lazima yakome.

Ameongea kuwa "Ikiwa ni pamoja na kiwango cha kutisha cha vifo vya watoto kaskazini mwa Gaza kutokana na mashambulizi mengine, matukio haya ya hivi karibuni yanachanganyika katika kuandika sura nyingine ya giza katika mojawapo ya vipindi vya giza zaidi vya vita hivi vya kutisha".

Bi. Russel ameonya kwamba "Wakazi wote wa Palestina kaskazini mwa Gaza, hasa watoto, wako katika hatari ya kufa kutokana na magonjwa, njaa na mashambulizi ya mabomu yanayoendelea."

Ameongeza kuwa UNICEF inaiomba Israel kufanya uchunguzi wa haraka kuhusu mazingira ya shambulio dhidi ya wafanyakazi wake na kwamba hatua zichukuliwe kuwawajibisha wale watakaobainika kuhusika.

Kutoa misaada wakati wa migogoro

Matukio hayo yalitokea wakati wa usitishaji uhasama uliokubaliwa kwa minajili ya kibinadamu, kuanzia saa kumi na mbili asubuhi hadi saa kumi jioni wakati wa kampeni ya siku tatu.

Polio ambayo ilitokomezwa huko Gaza miaka 25 iliyopita, iliibuka tena mapema mwaka huu katikati ya machafuko mengi ya kibinadamu yaliyosababishwa na vita, ambavyo vilianza kufuatia mashambulio mabaya ya Hamas dhidi ya Israeli Oktoba 2023.

Hadi sasa, vita vya Israel dhidi ya Gaza vimeua zaidi ya watu 43,000, kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza, na kuharibu maeneo makubwa ya Ukanda huo, ikiwa ni pamoja na vituo vya maji na vituo vya afya.

Licha ya changamoto za ufikiaji, Kamati ya Kiufundi ya Polio ya Gaza, ambayo inajumuisha wizara ya afya ya Palestina, shirika la WHO, UNICEF, na shirika la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA na washirika wengine, iliamua kurejesha kampeni hiyo, ambayo ilikuwa imeahirishwa tangu Oktoba 23 kutokana na ukosefu wa hakikisho la usalama.

Mapema Jumamosi asubuhi, timu 216 zilitumwa katika maeneo 106, 22 kati yao yakiwa yameongezwa ili kuhakikisha ongezeko la upatikanaji wa chanjo katika maeneo ambayo watu waliokimbia makazi yao hivi karibuni wanatafuta hifadhi, kulingana na mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Kwa kuongezea, zaidi ya "wahamashishaji 200 wa kijamii walishirikisha jamii na kukuza uelewa kuhusu juhudi za chanjo.”

Wafanyakazi wa UNRWA wanaendelea kufanya kazi huko Gaza inapowezekana.
© UNRWA
 
Wafanyakazi wa UNRWA wanaendelea kufanya kazi huko Gaza inapowezekana.

Lengo linakaribia kukamilika

Kampeni hiyo kaskazini mwa Gaza inafuatia kutekelezwa kwa mafanikio kwa awamu mbili za kwanza za duru ya pili ya kati na kusini mwa Gaza, ambayo ilifikia watoto 451,216, au jumla ya asilimia 96 ya lengo katika maeneo haya.

Ili kukomesha virusi vya polio vinavyoenea kwa urahisi, angalau asilimia 90 ya watoto wote katika kila jamii na mitaa lazima wapatiwe chanjo, kwa mujibu wa WHO.

Kucheleweshwa kwa kutoa dozi ya pili ya nOPV2 ndani ya wiki sita kunapunguza athari chanya za raundi mbili za karibu, na kupunguza kinga, limesema shirika hilo la Umoja wa Mataifa.

WHO pia imeonya kwamba kuwa na idadi kubwa ya watoto wanaokosa chanjo yao ya pili kunahatarisha sana juhudi za kukomesha kuenea kwa virusi hivyo  vya polio na kunaweza kusababisha wagonjwa zaidi katika Ukanda wa Gaza na nchi jirani.

No comments