COP29: Washiriki watakiwa kuacha maigizo, wajikite kwenye mambo ya msingi

Mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP29 ukiingia katika wiki yake ya mwisho huko Baku, Azerbaijan, Mkuu wa masuala ya tabianchi kwenye Umoja wa Mataifa Simon Stiell ametaka washiriki na wasuluhushi kujikita katika mambo ya msinig na kuibuka na makubaliano mapya ya ufadhili wa fidia kwa nchi zilizoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.
Malipo hayo yatawezesha nchi hizo kugharimia kipindi cha mpito cha kutumia nishati isiyoharibu mazingira, kama njia ya kuondokana na nishati kisukuku.
“Hatuwezi kuacha kuona msitu, kwa sababu tu tunajikita na mti mmoja mmoja” ameesma Stiell huku akisihi washiriki kukamilisha hoja ya msingi mapema wiki hii, ili kuwe na muda wa kutosha wa kupitisha maamuzi ya kisiasa.
COP29 ilianza huko Azerbaijan Jumatatu iliyopita ikiwa na lengo kuu la kufikia makubaliano ya kungeza ufadhili wa kutatua madhara makubwa ya ongezeko la joto duniani.

Licha ya mwelekeo mzuri wa mapema kuhusu viwango vitakavyofungua njia ya mfumo unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa wa biashara ya hewa ya ukaa, mazungumzo kuhusu ufadhili kwa tabianchi yamesuasua huku washiriki wakijikita kwenye mambo mengine badala ya kusaka makubaliano ya pamoja.
“Ulaghai, kucheza na hatari na maigizo,” vinazidi kupoteza muda muhimu na kutowesha nia njema inayohitajika kwa ajili ya makubaliano yenye mipango ya juu amesisitiza Bwana Stiell ambaye ni Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa MAbadiliko ya Tabianchi, UNFCCC, ambayo ndio huitisha mikutano ya COP.
Hali ni tete kwenye suala la “mlipuko wa kujifikiria kwanza ambako makundi ya kila pande yanajiangalia yenyewe na kukataa kusongesha suala, hadi wengine wasongeshe kwingineko,” amesema na kuongeza kuwa “njia pekee ya kutekeleza jambo ni “pale pande zimejiandaa kusonga mbele kwa pamoja na kufikia msimamo mmoja.”
Ombi la Stiell linakuja baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kuonesha pia wasiwasi wake juu ya hali ya mashauriano COP29, akieleza kuwa pande husika zinapaswa kuwa na mapendekezo ya juu kwenye lengo la ufadhili kwa tabianchi ili kuendana sambamba na changamoto zinazokabili nchi zinazoendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari huko Rio de Janeiro, Brazili kabla kuanza kwa G20 jana Jumapili, Guterres alisema “sasa ni wakati wa nchi zenye uchumi wa juu na zinazoongoza kwa kutoa hewa chafuzi kuongoza kwa mfano. Kushindwa si mbadala.

‘Hakuna uamuzi bila sisi’
Kando mwa mashauriano na mazungumzo yanayoendelea, mikutano mingine imeendelea kuanzia tabianchi na afya, hadi maendeleo ya binadamu na elimu.
Watoto na vijana walipaza sauti zao katika mikutano iliyokuwa imejaa hamasa wakitaka ulinzi kuanzia madhara ya mabadiliko ya tabianchi; mikakati ya kuzuia uharibifu zaidi wa sayari dunia na juhudi za kulinda mazingira.
Wamesihi wapitisha maamuzi kuwapatia kiti katika mashauriano ya mabadiliko ya tabianchi na kuandaa mkutano mahsusi wa Umoja wa Mataifa kuhusu tabianchi ukileta watoto peke yao.
Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, mabadiliko ya tabianchi yanadhuru ustawi wa watoto bilioni moja, nusu yao watoto duniani. Uchafuzi wa hewa, magonjwa ya kuambukiza, uharibifu wa mazingira na matukio ya kupitiliza ya hali ya hewa yanadhuru afya ya watoto, yanakwamisha elimu yao, na kuwanyima lishe bora wanayohitaji ili wakue vema.

Wakati wa mkondo joto mkali, watoto wanakuwa hatarini kukosa maji mwilini, miili yao haiwezi kudhibiti joto kwa ufanisi. Mafuriko na ukame huzorotesha familia na kuacha watoto wakiwa na madhara zaidi.
“Mafuriko yanasababisha shule kufungwa Liberia, na watoto hawaendi shuleni,” amesema Juanita Tamba, kutoka Shirikisho la Skauti wa Kike na watoto wa kike duniani, WAGGGS, moja ya shirika kubwa la kujitolea la kusongesha haki za wanawake na watoto duniani.
“Na wakati wa ukame, tunasafiri umbali mrefu kwenda kuteka maji, na watoto wa kike mara nyingi wanakumbwa na ghasia na ukatili wanapojaribu kwenda kuteka maji,” amesema Juaniti akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa Baku.
Chanzo UN
No comments