COP29: Sasa ni wakati wa kusonga mbele kuacha uchafuzi na si kurudi nyuma

Tunahitaji juhudi kubwa za kimataifa kuelekeza dunia yetu kwenye njia salama; ninyi mko mstari wa mbele kusaidia walaji, wawekezaji na wasimamizi wa kanuni wafahamu maana ya kuondokana na hewa chafuzi. Ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres aliyotoa leo huko Baku, Azerbaijan.
Amesema hayo alipokutana na wawakilishi wa taasisi zisizo za kiserkali wanaoshiriki mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP29.
Guterres alikuwa anagusia dhima muhimu ambayo majiji, maeneo mbali mbali, taasisi za biashara na fedha zinapaswa kutekeleza ili kuchagiza juhudi za dunia za kufikia kuondokana na utoaji wa hewa chafuzi ifikapo katikati ya karne hii yaani mwaka 2050.
Wakati huu ambapo matukio mabaya ya kupitiliza ya hali ya hewa yakileta madhara kwa binadamu na uharibifu wa kiuchumi duniani kote, na juhudi za kudhibiti wastani wa ongezeko la joto usizidi nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi, Guterres aliamua tangu mwaka 2022 awe anaitisha mkutano na taasisi zisizo za kiserikali, kwa mujibu wa mapendekezo ya ripoti iliyozinduliwa wakati wa COP27 huko Sharm-el-Sheikh.

‘Mwelekeo wa njia salama’
Ripoti hiyo, Uadilifu ni muhimu, iliweka mapendekezo 10 ambayo yaneonesha jinsi ya kuelekeza kuwa na ahadi wajibifu na halisia za kuondokana na utoaji wa hewa chafuzi.
Mapendekezo yanaainisha ni jambo gani taasisi zisizo za kiserikali zinaweza kuzingatia katika kila hatua kuelekea kufanikisha ahadi za kuondokana na hewa chafuzi na kutatua janga la tabianchi.
Kwa urahisi tu, kuondokana na hewa chafuzi kunamaanisha kuweko kwa mizania kati ya kiwango cha hewa chafuzi inayozalishwa na kiwango cha hewa chafuzi kinachoondolewa kwenye anga. Kufikia lengo hili kunahitaji ushirikiano kati ya taasisi za fedha na za kibiashara, halikadhalika na taasisi nyingine zinazoshirikiana na serikali.
‘Kusonga mbele na si kurudi nyuma’
Katibu Mkuu pia ameshukuru taasisi hizo zisizo za kiserikali kwa kuchukua jukumu ongozi la juhudi za kimataifa za kuondoa hewa chafuzi, lakini amesema “sasa tunahitaji wengine wafuate.”
Kwanza amesihi taasisi hizo kuwa zimeandaa mipango thabiti ya mpito na wajibifu ifikapo COP30 hapo mwakani. Mipango hiyo lazima iendane na kudhibiti wastani wa joto usizidi 1.5C, na pia waweke mwelekeo wa kutokuweko kwa hewa chafuzi ifikapo 2050 kupitia 2025, 2030, 2035, na zaidi.
“Lazima waweke njia ya kuondokana na nishati kisukuku – kwa kuzingatia sayansi. Lazima waweke bayana sera za ushawishi na ushirikishi. Na lazima waahidi kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa katika mnyororo mzima wa thamani,” amesema Guterres.
Amesema mipango hiyo isiwe yenye hila inayoficha uchafuzi kama vile uchafuzi utokanao na utupaji wa takataka.
“Sasa ni wakati wa kusonga mbele na si kurudi nyuma; ni wakati wa kuweka matarajio makubwa na uwazi. Hakuna hila au kuficha uchafuzi,” amesisitiza.

Kushirikiana na serikali
Bwana Guterres ametaka kuondokana na ahadi za hiari na kwenda kwenye ahaid za lazima. “Mustakabali wa ubinadamu uko mashakani. Hatua haziwezi kuwa mbadala. Kuweka bayana mipango ya mpito inayozingatia kutoongeza wastani wa joto kwa nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi iwe ni jambo la lazima kwa kampuni na taasisi za fedha.”
Mkuu huyo wa UN pia amesihi sekta za biashara, taasisi za fedha, majiji na maeneo mbali mbali kushirikiana zaidi na serikali katika mipango yao ya kitaifa ya kukabili madhara ya tabianchi, NDCs, inayotarajiwa kuwasilisha COP30.
“Saidieni serikali kuhakikisha kuwa zinawasilisha sera na uhakika wa usimamizi na ufuatialiaji wa nyuzijoto 1.5. Lazima tuhakikishe serikali zinawezesha kazi za pande nyingine kwenye suala hili, badala ya kufanya kazi kuwa ngumu kwa wale wanaotaka kuzingatia lengo hili la 1.5.
Chanzo UN
No comments