Wahusika wa ukatili dhidi ya wapalestina na waisraeli wawajibishwe - Türk

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu hii leo imechapisha ripoti kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu huko Gaza, tangu Hamas washambulie Israeli Oktoba 7, 2023, jambo lililosababisha Israeli kujibu mashambulizi na sasa vita inaendelea hadi leo hii.
Tukio hilo lilisababisha vifo vya zaidi ya waisraeli 1,000 na wenginze zaidi ya 200 kutekwa nyara, na kisha hatua ya Israeli kujibu mashambulizi imesababisha hadi leo hii zaidi ya wapalestina 43,000 wameuawa Gaza, kwa mujibu wa mamlaka za eneo hilo.
Uchambuzi wa kina kwenye ripoti hiyo unaangazia kipindi cha miezi sita kuanzia Novemba 2023 hadi Aprili 2024, ikimulika mauaji ya rai ana ukiukwaj iwa sheria ya kimataifa ,mambo ambayo yanaweza kuwa uhalifu wa kivita dhidi ya binadamu au mauaji ya kimbari

Tofauti za mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu.
Iwapo vitendo hivyo vilitekelezwa kama sehemu ya mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya raia, yakitekeleza sera ya serikali au shirika, ukiukwaji huo unaweza kuwa uhalifu dhidi ya binadamu.
Na iwapo mauaji yametekelezwa kwa nia ya kusambaratisha kabisa au sehemu ya taifa, kabila, rangi au kundi la kidini, hiyo inaweza kuwa mauaji ya kimbari.
Ripoti iliyotolewa leo ina wasiwasi kuhusu:
- Hatua zinazochukuliwa na jeshi la Israeli, (IDF) ikiwemo kulazimisha watu kuhama, mashambulizi ya hospitali na waandishi wa habari.
- Ripoti ya matumizi ya silaha zenye madini ya fosiforasi nyeupe (wihte phosphorus) ambazo zimepigwa marufuku.
- Ukiukaji wa kanuni za vita ambazo zimekuwa zinazingatiwa kwa zaidi ya miaka 160.
Mathalani ripoti inasema kuwa “njia ambazo pande kinzani kwenye vita Gaza wameendeleza uhasama wao zimesababisha machungu makubwa, hasa kutokana na uamuzi wa Israeli wa kuendesha operesheni zake za kivita, na katika matukio mengi zimesababisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, halikadhalika ukiukwaji wa sheria ya kimataifa ya ubinadamu.

Kauli ya Türk
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu Volker Türk amenukuliwa akisema, “Nimeonya mara kwa mara kuhusu hatari ya uhalifu wa kikatili unaotekelezwa.”
Amesema haki lazime itendeke kwa ukiukwaji huo wa sheria ya kimataifa.
“Vita lazima ikome mara moja, mateka na wale waliokamatwa kiholela waachiliwe huru, na tujikite sasa katika ‘kumimina’ misaada ya kibinadamu Gaza,” amesema Kamishna Volker Türk.
Katika ripoti hiyo ya kurasa 32, Kamishna huyo amesisitiza umuhimu wa uzingatiaji haraka wa sheria za kimataifa.
No comments