Utekelezaji wa Azimio la Kisiasa dhidi ya usugu wa dawa kwa vimelea wamulikwa Jeddah

Miezi michache baada ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kupitia Azimio la Kisiasa la kukabili usugu wa dawa dhidi ya vimelea vya magonjwa , AMR, huko Jedda, Sauti Arabia kumeanza mkutano wa 4 wa kimataifa wa mawaziri dhidi ya usugu huo unaotishia mustakabali wa afya na maendeleo duniani.
Lengo ni kusongesha utekelezaji wa azimio hilo ambapo wawakilishi wa nchi 57 wakiwemo wa serikali, mashirika ya kiraia na wanazuoni pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa wanamulika jinsi ushirikiano mtambuka unavyoweza kukabili usugu wa dawa kwa vimelea ambao unaathiri afya, uchumi na jamii hasa za nchi za kipato cha chini na kati.
Akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa kwenye mkutano huo, Julian Nyamupachitu, Naibu Mkurugenzi wa ReAct Africa, mtandao wa kimataifa unaochagiza hatua dhidi ya AMR kwenye nchi za kipato cha chini na cha kati, amesema ugumu wa tatizo hilo unachochewa na ukata na ukosefu wa utashi wa kisiasa miongoni mwa viongozi.
Amesema huku kukiwa na changamoto lukuki za kiafya ambazo serikali zinakabiliana nazo, imekuwa vigumu sana kuhamisha maneno kutoka kwenye nyaraka kwenda kwenye utekelezaji.

Amesema kadri nchi zinapitia na kuchambua mipango yao ya kitaifa, ReAct Africa inazisaidia kupatia kipaumbele shughuli ambazo zina maana zaidi na zinatekelezeka, na kutumia mbinu walizo nazo ili kuchangia katika utungaji wa sera, mbinu kama vile Mbinu ya WHO ya gharama na bajeti.
Naibu Mkurugenzi huyo wa ReAct Africa amesema Azimio la Kisiasa la mwaka huu lilikuwa bora zaidi kuliko lililotangulia la mwaka 2016, lakini itakuwa vema sana kuona ahadi zaidi ya malengo kwenye suala la ufadhili.
Bi. Nyamupachitu amesema maudhui ya mkutano wa Jedddah ambayo ni Kutoka kwenye Azimio kuelekea kwenye Utekelezaji yamekuja wakati muafaka na matarajio yake ni kuona siku tatu za mkutano huo wa mawaziri zinamalizika na ahadi dhahiri.
“Naamini hamasa tayari imeongezeka. Wameshukuru takwimu walizopatiwa. Bila shaka ni tishio la dunia, na si kwa sekta ya afya tu, au kilimo pekee, au mazingira pekee na sekta ya Wanyama, bali ni tatizo la kiuchumi vile vile,” amesema Bi. Nyamupachitu.
No comments