Chalinze wataka mgao wao kutoka Bagamoyo

MADIWANI wa Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wametaka suala la mgawanyo wa mapato kumalizwa baada ya Halmashauri hiyo kujitoa kutoka Halmashauri mama ya Bagamoyo na kujitegemea.
 
Wakizungumza kwenye kikao cha madiwani cha kupokea taarifa ya mwaka mwaka kilichofanyika Lugoba walisema kuwa suala hilo limekuwa na utata mkubwa hali ambayo inasababisha miradi mingi kushindwa kufanyika kutokana na kusubiri fedha ambazo zinatokana na mgawanyo wa Halmashauri hizo.
 
Akizungumzia suala hilo Diwani wa kata ya Lugoba Rehema Mwene alisema kuwa kama suala hilo linakuwa gumu ni vema likapelekwa kwa ngazi ya mkoa ili Halmashauri yao ipate haki yao baada ya wao kujitenga na kuanzisha Halmashauri ya Chalinze.
 
“Tangu Halmashauri yetu ianzishwe kutoka Bagamoyo kwa sasa ni karibu mwaka lakini suala la mgawanyo limekuwa gumu hasa kwa upande wa fedha hali inayofanya miradi mingi ishindwe kufanyika kutokana na kutopata mgao wa fedha,” alisema Mwene.
 
Alisema kuwa lengo ni kupewa haki yao kwani wao kujitenga na Bagamoyo isiwe tatizo kwani hiyo ni sehemu ya kuharakisha maendeleo kwa wananchi hivyo ni vema wakapata kile wanachostahili kama sheria zinavyosema ambapo ni mradi mmoja tu uliotekelezwa wa madarasa ya shule za sekondari ambazo hata hivyo hazijakamilika.
 
“Ni vema suala hili lipelekwe mkoani na kama litakosa ufumbuzi lifikishwe kwa Waziri mwenye dhamana ili alipatie ufumbuzi kwani sula hili ni la kisheria ambapo baada ya kugawana mali tatizo limebaki kwenye fedha ambazo wao wangezitumia kama salio anzia,” alisema Mwene.
 
Kwa upande wake diwani wa kata ya Miono Juma Mpwimbwi alisema kuwa miradi mingi iliyokuwa upande wa Chalinze haijakamilika kutokana na fedha za kutekeleza miradi hiyo kutowasilihswa licha ya kufanyika mgawanyo huku ule wa fedha ukiwa bado haujafanyika.
 
Mpwimbwi alisema kuwa mfano wa miradi ambayo imekwama ni pamoja na masoko ambayo kwa sasa ujenzi wake umeishia katikati kuna haja ya halmashauri ya Bagamoyo kukamilisha mgawanyo huo wa fedha ambao umebakia ili mambo yaendelee.
 
Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze Saidi Zikatimu alisema kuwa halmashauri walisema kuwa hawawezi kutoa salio anzia kutokana na kutofunga taarifa ya mwaka ambayo wameifanya hivi karibuni na kuamini kuwa watafanikisha zoezi lililobaki.
 
Zikatimu alisema kuwa kikao cha mkoa kinatarajiwa kufanyika katikati ya mwezi huu hivyo wataliwasilisha jambo hilo ili liweze kupatiwa ufumbuzi ambapo fedha hizo zitatumika kwa ajili ya shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na malipo kwa watumishi wapya na watendaji mbalimbali wa Halmashauri.
 

No comments