Tume ya Mufti yaita wenye ushahidi, wezi wa mali za BAKWATA


Tume iliyoundwa na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zuberi kuchunguza
mali za Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), imeomba watu wenye
taarifu juu ya ubadhirifu wa mali za taasisi hiyo wawasiliane nao.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Makamu
Mwenyekiti wa tume hiyo, Sheikh Issa Othman Issa aliomba pia ushirikiano wa
watu wenye taarifa juu ya mali za baraza hilo.
Sheikh Issa aliahidi kuwa tume yake itawalinda wale wote watakaowapa taarifa
zozote zitakazosaidia katika uchunguzi wao.

“Tunaendelea kuwaomba wale wenye taarifa za mali za Waislamu ambazo ziko
chini ya usimamizi wa Bakwata wawasiliane na tume ikiwamo kukabidhi
nyaraka zote walizonazo, hata wenye ushahidi wowote wa ubadhirifu wa mali
wazilete tunaahidi kwa dhati tutazifanyia kazi na kuwalinda watoa taarifa, tume
hii ni huru ina ruhusa ya kuendesha kazi zake bila kuingiliwa na mtu ama
chombo chochote,” alisema Sheikh Issa.

Alisema katika kufanikisha kazi hiyo waliyopewa, tume hiyo inafanya kazi na
jopo la wataalamu na vyombo mbalimbali vilivyobobea katika masuala hayo.
Sheikh Issa alisema wamepewa hadidu za rejea saba ikiwamo kuchunguza
misamaha ya kodi iliyotolewa kwa baraza na taasisi zake.

Kuundwa kwa tume hiyo ni matokeo ya ushauri uliotolewa na Rais John
Magufuli, Julai mwaka huu alipokuwa akihutubia Baraza la Eid ambapo pia
aliahidi kuzirejesha mali zilizoporwa za waumini wa dini hiyo.

Sheikh Issa alisema kuwa wamepewa miezi mitatu kukamilisha uchunguzi huo.
Alitaja mambo watakayochunguza kuwa ni pamoja na misamaha ya kodi
iliyoombwa na Bakwata nchi nzima, mikataba yote ya uuzaji wa viwanja na
mali mbalimbali za baraza na taasisi zake pamoja na uhalali wa umiliki wake.

Nyingine ni kutafuta mikataba yote ambayo baraza na taasisi zake zimeingia na
wawekezaji na kuona mikataba hiyo kama ina maslahi na baraza au laa, na
kuchunguza mikataba yote ambayo taasisi zake nchi nzima zimeingia na
wapangaji wake katika maeneo mbalimbali yanayomilikiwa na baraza hilo.

Nyingine ni kuchunguza mali zote za baraza na kuona hali ya usajili wa mali
hizo na kuchunguza mapato na matumizi ya baraza hilo na taasisi zake nchi
nzima.

Sheikh Issa alisema baada ya uchunguzi huo kukamilika ndani ya siku hizo 90
watakabidhi ripoti hiyo kwa Mufti kwa ajili ya hatua nyingine zaidi.
Wakati huo huo, swala ya Eid El-Hajj inatarajiwa kuswaliwa leo makao makuu
ya Bakwata, yaliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jana na Katibu wa
Baraza hilo, Salim Abeid, swala hiyo itaambatana na Baraza la EID na kufuatiwa
na uzinduzi wa Chuo cha Kiislam.
Abeid alisema swala hiyo itafanyika saa moja na nusu asubuhi na mgeni rasmi
anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.






No comments