Wapalestina waendelea kufurushwa miaka 77 baada ya Nakba huku njaa ikishika kasi: UN
Wapalestina waendelea kufurushwa miaka 77 baada ya Nakba huku njaa ikishika kasi: UN
Wakati dunia ikiadhimisha miaka 77 tangu Nakba ambapo zaidi ya Wapalestina 700,000 walifurushwa kutoka vijiji na miji yao mwaka 1948 Shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limetoa onyo kali kuhusu sura mpya ya mateso na ufurushwaji wa lazima uonaoendele Gaza.
Tangu kuanza kwa mapigano ya sasa, takriban asilimia 90 ya watu wa Gaza wamelazimika kukimbia makazi yao, na familia nyingi zikiripoti kuwa zimeshahama zaidi ya mara kumi. “Baadhi yao wameshahama mara 10 au zaidi,” imesema UNRWA ikiongeza kuwa “Wapalestina bado wanafurushwa kwa nguvu, miaka 77 baada ya Nakba.”
Kwa mujibu wa shirika hilo miongoni mwa waathirika wakubwa ni watoto. Katika ujumbe uliogusa mioyo ya wengi, UNRWA imemwelezea Youssef, mtoto wa miaka 4 aliyedhoofika kwa utapiamlo mkali na majeraha.
“Hana chakula wala huduma za matibabu,” imesema UNRWA. “Watoto wangapi zaidi kama Youssef wanapaswa kuhukumiwa kifo ili kuondoa mzingiro wa Gaza? Hili linahitaji uamuzi wa kisiasa tu.”
UNICEF: Watoto 71,000 wahitaji matibabu ya haraka dhidi ya utapiamlo
Kwa mujibu wa ripoti mpya ya kutathimini viwango vya njaa IPC inayoungwa mkono na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, takriban watoto 71,000 huko Gaza wanahitaji matibabu ya dharura dhidi ya utapiamlo mkali.
UNICEF imetoa video ikionyesha juhudi zake za kukabiliana na hali hii, licha ya mazingira magumu ya kazi.
Takwimu kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu na masuala ya Dharura OCHA, zinaonesha hali inayoendelea kuzorota.
Wiki kumi baada ya kuwekewa vizuizi kamili vya misaada, Gaza bado haipokei chakula, mafuta, wala dawa imesema ofisi hiyo.
Idadi ya milo ya moto inayotolewa kila siku kupitia majiko ya kijamii imeporomoka kutoka milioni moja hadi milo 249,000 pekee.
“Watu wamejaa hofu na kila siku wananiambia hawajui wataishi vipi,” amesema Olga Cherevko, msemaji wa OCHA aliyepo Gaza.
Ameongeza kuwa “Nimepita katika baadhi ya majiko hivi karibuni ambapo mamia ya watu wamesimama na mabakuli matupu na huzuni usoni, na waliambiwa waende nyumbani kwa sababu chakula cha siku hiyo kilikuwa kimekwisha.”
Wito wa UN: ondoeni vikwazo ruhusuni msaada
Kadri hali ya kibinadamu inavyozidi kuwa mbaya, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanatoa wito wa kuchukuliwa hatua za dharura kuondoa vizuizi, kuruhusu misaada kuingia bila vikwazo, na kusitisha mzunguko wa watu kufurushwa na mateso.
“Nakba siyo historia ya zamani tu,” UNRWA imehitimishataarifa yake na kuongeza kuwa “Kwa Wapalestina wa Gaza, ni uhalisia wa kila siku.”
No comments