Mataifa yapitisha ahadi ya kihistoria ya kujikinga dhidi ya majanga ya magonjwa kwa siku zijazo

Mataifa yapitisha ahadi ya kihistoria ya kujikinga dhidi ya majanga ya magonjwa kwa siku zijazo

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Ghana, Charles Abani, anapokea chanjo ya COVID-19. (Maktaba)
UN Ghana
Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Ghana, Charles Abani, anapokea chanjo ya COVID-19. (Maktaba)

Baada ya miaka mitatu ya majadiliano yaliyochochewa na janga la COVID-19, nchi zimepitisha rasmi makubaliano ya kwanza kabisa ya kimataifa ya kuzuia, kujiandaa, na kukabiliana vyema na majanga ya magonjwa kwa siku zijazo. Mkataba huu mpya ni hatua kubwa kuelekea ushirikiano wa kimataifa ulioboreshwa ili kulinda maisha na kuepuka madhara makubwa ya milipuko ya magonjwa kwa siku za usoni.

Athari za janga la coronavirus">COVID-19 bado zinaendelea kuhisiwa kote duniani. Takriban watu milioni saba walifariki, mifumo ya afya ililemewa, na uchumi wa dunia ulisimama kwa kiasi kikubwa.

Msukosuko huu wa kimataifa uliisukuma jumuiya ya kimataifa iliyokuwa na mshtuko kutafuta makubaliano ya kuzuia tukio kama hilo la kutisha kutokea tena — na kuhakikisha dunia ina maandalizi bora zaidi kwa siku zijazo.

Uamuzi huu wa kihistoria umefanyika katika Mkutano wa 78  wa Baraza la Afya la Umoja wa Mataifa,(WHA) mkutano wa kila mwaka wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) ulioanza  tarehe 19 Mei na utaendelea hadi tarehe 25 mwezi huu jijini Geneva, Uswisi.

Ingawa kupitishwa rasmi kumefanyika leo Jumanne, Nchi Wanachama wa WHO wameidhinisha makubaliano hayo kwa wingi siku ya Jumatatu jana Mei 19 (kura 124 za kuunga mkono, hakuna pingamizi, watu 11 walijizuia kupiga kura).

“Mkataba huu ni ushindi kwa afya ya umma, sayansi na hatua za pamoja za kimataifa,” ametangaza Daktari Tedros Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO na kuongeza kuwa “utawezesha sisi, kwa pamoja, kulinda dunia vyema dhidi ya vitisho vya majanga ya magonjwa ya baadaye. Ni pia kutambuliwa na jumuiya ya kimataifa kuwa raia wetu, jamii na uchumi visiachwe kuwa dhaifu na kupitia mateso kama yale ya COVID-19.”

Nchi Wanachama wa WHO ziliidhinisha Mkataba wa kwanza kabisa wa udhibiti wa magonjwa ya milipuko tarehe 19 Mei 2025
WHO/Christopher Black
Nchi Wanachama wa WHO ziliidhinisha Mkataba wa kwanza kabisa wa udhibiti wa magonjwa ya milipuko tarehe 19 Mei 2025

‘Fursa ya mara moja maishani’

Janga la COVID-19 lilidhihirisha tofauti kubwa za upatikanaji wa vipimo, matibabu na chanjo kati ya nchi na ndani ya nchi, na lengo kuu la mkataba huu ni kuziba mapengo haya na kuhakikisha majanga ya magonjwa kwa siku za usoni yanashughulikiwa kwa usawa na kwa ufanisi zaidi.

“Sasa kwamba Mkataba umeanzishwa, ni lazima sisi sote tuchukue hatua kwa haraka sawa kutekeleza vipengele vyake muhimu, ikiwemo mifumo ya kuhakikisha upatikanaji wa haki wa bidhaa za afya zinazohusiana na majanga ya magonjwa,” ametangaza Daktari Teodoro Herbosa, Katibu wa Wizara ya Afya ya Ufilipino na Rais wa Mkutano wa mwaka huu wa Afya Duniani, ambaye aliongoza mchakato wa kupitisha Mkataba huo.

“COVID ilikuwa dharura ya mara moja maishani, na Mkataba wa WHO kuhusu majanga ya magonjwa ni fursa ya mara moja maishani ya kujifunza kutoka kwenye janga hilo na kuhakikisha watu duniani kote wanalindwa vyema iwapo kutazuka pandemiki nyingine.”

Masuala ya mamlaka ya kitaifa

Suala la mamlaka ya kitaifa limeibuliwa mara kadhaa wakati wa majadiliano ya mkataba huo, jambo linalotokana na madai ya uongo mtandaoni kwamba WHO inajaribu kuchukua udhibiti kutoka kwa nchi binafsi.

Mkataba huu unasisitiza kwamba hilo si kweli, ukieleza kuwa hakuna kilicho ndani yake kinachotoa mamlaka kwa WHO kubadilisha au kuingilia sheria za kitaifa, au kulazimisha mataifa kuchukua hatua kama kupiga marufuku wasafiri, kutoa chanjo kwa lazima au kuweka vizuizi vya kutotoka nje.

Nchi Wanachama wa WHO ziliidhinisha Mkataba wa kwanza kabisa wa udhibiti wa magonjwa ya milipuko tarehe 19 Mei 2025
WHO/ Christopher Black
Nchi Wanachama wa WHO ziliidhinisha Mkataba wa kwanza kabisa wa udhibiti wa magonjwa ya milipuko tarehe 19 Mei 2025

Hatua zinazofuata

Kupitishwa kwa mkataba huu kumesifiwa kama hatua ya msingi, lakini huu ni mwanzo tu wa mchakato.

Hatua inayofuata ni kuanza utekelezaji wa makubaliano hayo kwa kuanzisha mchakato wa kuandika na kujadiliana kuhusu mfumo wa Ushirikishanaji wa Vimelea vya magonjwa na Faida (Pathogen Access and Benefit Sharing – PABS) kupitia Kundi la Kazi la Kiserikali.

Matokeo ya mchakato huu yatapitiwa katika Mkutano Mkuu wa Afya wa mwaka ujao.

Mara baada ya Mkutano wa Afya Duniani kupitisha Mfumo wa PABS, mkataba utawekwa wazi kwa kutiwa saini na kuanza mchakato wa kuridhiwa, ikiwemo kupitia mabunge ya kitaifa. Ukisharidhiwa na nchi 60, utaanza kutumika rasmi.

Vipengele vingine ni pamoja na kuanzishwa kwa utaratibu mpya wa kifedha kwa ajili ya kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na majanga ya magonjwa, na kuundwa kwa Mtandao wa Kimataifa wa Ugavi na Usambazaji ili “kuboresha, kuwezesha, na kuondoa vikwazo kuhakikisha upatikanaji wa haki, kwa wakati, kwa haraka, salama na kwa bei nafuu wa bidhaa za afya zinazohusiana na majanga ya magonjwa kwa nchi zinazohitaji wakati wa dharura za afya za kimataifa, zikiwemo majanga ya magonjwa na kwa ajili ya kuzuia dharura hizo.”

No comments