Mashambulizi kwa kutumia ndege zisizo na rubani Sudan, UN inaendelea kufuatilia hali
Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Stephanie Trambley, ambaye ni mmoja wa maafisa wa Ofisi ya Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amewaeleza waandishi wa Habari jijini New York-Marekani kwamba Umoja wa Mataifa unaendelea kufuatilia kwa karibu hali.
Ameeleza pia kuwa Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura, OCHA, Tom Fletcher, ana wasiwasi kuhusu mashambulizi ya ndege ndogondogo yanayoendelea mjini Port Sudan, “ambao kama mnavyofahamu ni kitovu cha shughuli zetu za misaada ya kibinadamu na lango kuu la kuingiza misaada."
Fletcher anasisitiza umuhimu wa kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu, akieleza kuwa “lazima tahadhari ya hali ya juu ichukuliwe ili kulinda raia na miundombinu ya kiraia.” Mashambulizi haya yamesababisha kusimamishwa kwa safari za Shirika la Huduma za Anga la Umoja wa Mataifa (UNHAS) kwenda na kutoka Port Sudan tangu Mei 4 — huduma muhimu kwa usafirishaji wa misaada na watendaji wa kibinadamu.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), linalosimamia UNHAS, limesema kuwa safari hizo zitaanza tena “mara hali itakaporuhusu,” lakini hali ya sasa ya usalama inadhoofisha sana uwezo wa kufikisha misaada kwa maeneo mengi.
Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imeripoti kuwa mashambulizi ya ndege ndogondogo zisizo na rubani yameenea hadi majimbo ya Kassala na Nile ya Kaskazini. Huko Kassala, mashambulizi karibu na uwanja wa ndege mapema wiki hii yalisababisha watu wapatao 2,900 kukimbia makazi yao na shughuli za misaada kulazimika kusitishwa au kuhamishwa kwa muda.
Katika Jimbo la Nile ya Kaskazini, shambulio la Aprili 25 kwenye kituo cha transfoma mjini Atbara lilisababisha kukatika kwa umeme, jambo ambalo limechangia upungufu wa mafuta na mkate, na kusababisha misururu mirefu kwenye vituo vya mafuta na mikate.
“Mvurugano huu si tu wa usafirishaji,” amesema msemaji wa Umoja wa Mataifa. “Unahatarisha maisha ya watu kwa kuchelewesha upatikanaji wa chakula, dawa, na misaada mingine muhimu kwa wale wanaohitaji sana.”
Huku hali ikiendelea kubadilika, Umoja wa Mataifa umerejea tena wito wake kwa pande zote zinazohusika na mzozo kuheshimu sheria za kimataifa na kuhakikisha ulinzi wa wahudumu wa misaada na miundombinu ya kibinadamu.
“Tunaendelea kufuatilia hali kwa karibu,” Stephanie amesema na kuongeza kuwa, “Timu zetu zinajitahidi kurejesha shughuli za misaada haraka iwezekanavyo, lakini usalama wa wafanyakazi wetu na watu tunaowahudumia ni wa kipaumbele.”
No comments