Port Sudan: Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yaendelea, Mkuu wa UN atoa wito wa amani
Port Sudan: Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yaendelea, Mkuu wa UN atoa wito wa amani
Hali ya usalama katika mji wa Port Sudan nchini Sudan imeendelea kuzorota kutokana na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani au dironi yaliyofanywa na vikosi vya kijeshi vya Msaada wa Haraka RSF.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres mashambulizi haya yameathiri vibaya miundombinu muhimu, ikiwa ni pamoja na viwanja vya ndege, bandari, na vituo vya mafuta, na kusababisha uharibifu mkubwa na kuathiri utoaji wa misaada ya kibinadamu.
Kupitia taarifa yake iliyotolewa mjini New York Marekani Jumatano jioni Guterres ametoa wito wa dharura kwa mazungumzo ya amani ili kumaliza vita vinavyoendelea kwa zaidi ya miaka miwili nchini Sudan.
Bwana Guterres ameonya kuwa kuendelea kwa mzozo huo kunaweza kusababisha vifo vya raia kwa kiwango kikubwa na kuzidisha hali mbaya ya kibinadamu inayoshuhudiwa kote nchini.
Ameongeza kuwa "Kuenea kwa vita hadi maeneo ambayo yanatoa hifadhi kwa maelfu ya watu waliofurushwa makwao ni jambo la kutia wasiwasi mkubwa,"
Wito wake unakuja baada ya siku kadhaa za mashambulizi ya droni kwenye miundombinu muhimu ya Port Sudan, mji ulio kando ya Bahari ya Shamu na unaotegemewa kwa usafirishaji wa misaada ya kibinadamu.
Mji huo pia unahifadhi mamia ya maelfu ya wakimbizi wa ndani na kwa sasa ndio makao ya serikali ya kijeshi baada ya kupoteza udhibiti wa mji mkuu Khartoum kwa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF)
Safari za ndege za misaada zasitishwa
Kufuatia mashambulizi hayo, Umoja wa Mataifa umesema safari za Shirika la Huduma za Anga la Umoja wa Mataifa UNHAS, kwenda na kutoka Port Sudan zimesitishwa tangu tarehe 4 Mei.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP, linalosimamia safari hizo, limesema kuwa huduma zitaanza tena pindi hali ya usalama itakaporuhusu.
Kwa sasa, milio ya risasi na silaha usiku kucha imeathiri sana harakati za wahudumu wa misaada kuingia Sudan na kusambaza misaada kote nchini.
No comments