Vijana vijiji watakiwa kutumia fursa za umeme wa jua kujiajiri
Arusha.Kampuni ya Kimataifa ya umeme wa jua ya Mobisol ya Ujerumani, imetoa fursa kwa vijana wa vijijini ambao maeneo yao hayana umeme,kujiajiri katika kazi za kunyoa, kutokana na kuanza kusambaza mashine zinazotumia umeme wa jua.
Meneja masoko wa kampuni hiyo,Demetrius Wiston akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema vijana wakitumia fursa zinazotokana na kampuni hiyo,wataweza kukabiliana na umasikini kwa kujiajiri wenyewe.
Alisema sambamba na huduma hiyo ya kunyoa, pia kampuni hiyo imeanza kusambaza luninga zinazotumia jua ambazo zinaweza kutumika kibiashara, mitambo ya kuchaji simu, radio na majokofu.
“huduma hii inapatikana katika mikoa 20 ambayo tunafanya kazi na lengo letu kuwa ni kufika vijiji vyote, maeneo ambayo jamii zipo nyuma”alisema
Waanzisha kampeni ya hamasika na masika.
Katika hatua nyingine, Kampuni hiyo,imeanzisha kampeni ya hamasika na masika, ambayo ina lengo la kuendesha bahati nasibu kwa wateja wake watakaonunua bidhaa mwezi April na Mei katika mikoa 20 na zawadi zenye thamani ya milioni 4 zitatolewa.
Meneja chapa na uwezeshaji wa Mobisol Seth Mathemu alisema zawadi mbali mbali ikiwepo fedha taslimu,pikipiki na nyingine zenye thamani ya zaidi ya Sh 4 milioni zitatolewa.
Alisema mikoa ambayo itakuwa katika promosheni hiyo ni Arusha, Kilimanjaro na Manyara,Singida, Dodoma, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mara, Kagera, Simiyu, Geita, Kigoma, Rukwa, Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe, Pwanipamojana Morogoro.
No comments