POLISI NANE WAUAWA KWA KUPIGWA RISASI PWANI...RAIS MAGUFULI AWALILIA

 Dar es Salaam. 

Rais John Magufuli amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya Askari Polisi wanane waliouawa kwa kushambuliwa na watu wenye silaha jana jioni katika eneo la Jaribu Mpakani, Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani.

Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu leo inasema askari Polisi hao walikuwa wakitoka kubadilishana doria wameshambuliwa kwa kupigwa risasi wakiwa wanasafiri kwa gari katika barabara ya Dar es Salaam – Lindi.

Mkuu wa jeshi la polisi Tanzania IGP Ernest Mangu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa taarifa zaidi zitatolewa na kamanda wa polisi mkoa wa Pwani.
Taarifa zinasema kuwa polisi hao walikuwa kwenye gari wakirejea kituoni kutoka kwenye doria na walishambuliwa na watu waliotokea msituni. 

Imeelezwa  kuwa majambazi hao waliwavamia ghafla polisi hao waliokuwa kwenye gari na kuwapiga risasi na kuwaua wote palepale eneo la tukio, kisha kutokomea kusikojulikana na kwamba silaha zote walizokuwa nazo (SMG) zilichukuliwa na watu hao.

Kutokana na tukio hilo, Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP-Ernest Mangu, familia za askari wote waliouawa, Askari Polisi wote na Watanzania wote walioguswa na vifo hivyo.

Rais Magufuli amelaani tukio hilo na matukio yote ya kuwashambulia askari polisi ambao wanafanya kazi kubwa na muhimu ya kulinda raia na mali na ametaka Watanzania wote watoe ushirikiano katika kukomesha vitendo hivyo


 

No comments