Sumatra kwa kushirikiana na Jeshi la polisi kikosi cha Usalama barabarani waanza kutoa Elimu juu ya usafirishaji wa mazao ya Misitu
Na,Vero Ignatus, Dar es salaam
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania
(TFS), Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama
Barabarani na Mamlaka ya Usafirishaji wa nchi Kavu na Majini (Sumatra) imeanza kampeni ya kutoa elimu juu ya njia halali za usafirishaji wa mazao ya misitu hususani mkaa katika barabara kuu zilizopo nchini kote.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Tulizo Kilaga alisema uvunaji holela na usafirishaji haramu wa mazao ya misitu hasa mkaa kwa kutumia pikipiki na baiskeli kutoka misitu ya hifadhi,mapori ya akiba na hata hifadhi za Taifa, unatajwa kuwa chanzo kikuu cha uharibifu wa misitu.
Kilaga alisema TFS imeamua kutoa elimu kwa umma kabla ya kuchua hatua za kusimamia sheria na kanuni za usafirishaji kwa lengo la kudhibiti uharibifu huo kabla nchi haijageuka
jangwa siku za karibuni.
Alisema Tanzania inakadiriwa kuwa na hekta milioni 48 za misitu ambapo jumla ya hekta 372,000 huaribiwa kwa mwaka.
Kiwango ambacho ni sawa na asilimia 1.1 ya eneo lote lenye misitu hapa nchini, na ni sawa na kufyeka zaidi ya hekta 1,000 kwa siku.
Aliongeza kuwa Jiji la Dar es Salaam peke
yake zaidi ya magunia 500, 000 ya mkaa
huingizwa katika kipindi cha mwezi mmoja na kuongeza kuwa inakadiriwa pikipiki 20 zikisafirisha mkaa ni sawa na lori moja la tani saba lililojaa mkaa, na njia hii ya usafiri wa mazao ya misitu kwa baiskeli na pikipiki inakiuka Mwongozo wa Uvunaji Endelevu wa Mazao ya Misitu, 2015 unaoeleza kuwa vyombo vya usafiri vinavyoruhusiwa kusafirsha mazao ya misitu ni vile vyenye magurudumu
manne.
Mkuu wa Kitengo cha Elimu, Makao Makuu ya Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mossi Ndozero alisema usafiri unaoendelea wa mazao ya misitu kwa baiskeli na pikipiki ni hatarishi na unaokiuka Sheria ya Usalama
Barabarani sura ya 168 iliyorejewa mwaka
2002 inayotambua pikipiki na baiskeli kama vyombo vya usafiri kwa ajili ya abiria na si kubeba mizigo.
Aidha, Kaimu Meneja wa Mawasiliano wa
Mamlaka ya Usafirishaji wa nchi Kavu na
Majini, Salum Pazi alisema kwa mujibu wa
Kanuni ya Leseni za Usafirishaji ya Sumatra, 2010 inatambua pikipiki kama chombo cha kusafirisha abiria na si vinginevyo.
No comments