Waziri Mkuu Ahimiza Matumizi Ya Mifumo Ya Ulinzi Wa Miji Ya Kielektroniki
Ametoa
agizo hilo jana (Alhamisi, Mei 24, 2018) wakati akizungumza na mamia
ya wananchi na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam na viongozi wa Jeshi la
Polisi kwenye viwanja vya Mbweni, wilayani Kinondoni, mkoani Dar es
Salaam baada ya kuzindua vituo vya polisi vya kisasa vya Mburahati,
Kiluvya-Gogoni na Mbweni.
“Katika
suala zima la kuimarisha usalama, napenda niwape changamoto Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi ili zitoe kipaumbele kwenye
matumizi ya City Surveilance System (CCTV). Usimikaji wa mifumo hiyo
utasaidia kupunguza uhalifu na kuongeza usalama wa wananchi na mali
zao,” amesema.
Waziri
Mkuu amesema tayari Jiji kama Nairobi la nchini Kenya linatumia mifumo
ya aina hiyo na kwamba uwepo wa mifumo hiyo, na haoni ni kwa nini
Tanzania bado haijawa na mifumo kama hiyo.
Amesema
uwepo wa mifumo hiyo, utasaidia si tu kutambua kwa wepesi wahusika wa
matukio ya uhalifu kama vile ukwapuaji, wizi wa magari na uharibifu wa
mali, bali pia utaongeza shughuli za kibiashara na utalii.
"Tanzania
hatujaanza kutumia mifumo hii lakini ifike mahali, tuanze kubadilika.
Tafuteni wataalamu wenye ujuzi watufungie mifumo hii ili iwe rahisi
kufuatilia matukio mbalimbali. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani fuatilia
mifumo hii ili tuanze na majiji yetu na tuweze kufuatilia matukio ya
kihalifu barabarani na mitaani", amesema Waziri Mkuu.
"Nitoe
rai kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi wachukue
hatua za haraka kurahisisha upatikanaji wa matumizi ya mifumo hiyo
hususan katika majiji yetu kwa ajili ya kuimarisha usalama wa watu na
mali zao," amesema.
Mapema,
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Yusuf Masauni
alimshukuru Rais Dkt, John Pombe Magufuli kwa kukubali kutoa kiasi cha
sh.bilioni 10 kwaajili ya ujenzi wa nyumba za polisi.
Alisema kutokana na fedha hizo, nyumba takriban 400 za askari polisi, zinatarajiwa kujengwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Akitoa
taarifa ya ujenzi wa vituo hivyo vitatu, Inspekta Jenerali wa Polisi,
Simon Sirro alisema ujenzi wa kituo cha Mburahati umegharimu sh. bilioni
1.2, Kiluvya (sh. milioni 227) na Mbweni (sh. milioni 667).
Alisema
ujenzi wa vituo hivyo umeshirikisha wananchi wa maeneo husika, Jeshi la
Polisi na wadau werevu ambao ni walipakodi wazuri na wazalendo zikiwemo
taasisi na watu binafsi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
No comments