BABA AMUUA MWANAYE KISHA KUMZIKA KISA KAJISAIDIA KILA MAHALI NDANI
Jeshi
la Polisi Mkoani Mwanza linamshikilia mwanaume mmoja kwa tuhuma za
mauaji ya mtoto wake wilayani Ukerewe mwenye miaka miwili baada ya
kumchapa fimbo sehemu mbalimbali za mwili kutokana na kujisaidia kinyesi
kwenye nyumba hali iliyopelekea kupoteza maisha.
Hayo
yamebainishwa na Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza Naibu Kamishina wa
Polisi Ahmed Msangi wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari
na kumtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Buyanza Magayane (39) ambapo baada ya
kufanya tukio hilo alimzika mtoto huyo aliyefahamika kwa jina la Baraka
Buyanza kwenye shamba lake lililopo nyuma ya nyumba yake, ambapo kitendo
hicho ni kosa kisheria.
Aidha,
Kamanda Msangi amesema inadaiwa mtuhumiwa huyo alikuwa ametengana na
mkewe yaani mama wa marehemu kwa muda mrefu, hivyo marehemu alikuwa
akiishi na baba yake mzazi anayetuhumiwa kusababisha kifo chake pamoja
na mama yake wa kambo.
Inasemekana
Mei 23, 2018 mtuhumiwa alikuwa ametoka kwenye shughuli zake za kila
siku ndipo aliporudi nyumbani, alimkuta marehemu akiwa amejisaidia
kinyesi katika sehemu tofauti tofauti za nyumba yake ndipo alipomchukua
kisha kumchapa kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na kumfungia
ndani ya chumba peke yake baada ya muda alipokwenda kumuangalia alimkuta
mtoto huyo ameshafariki.
Mbali
na hilo, Kamanda Msangi amesema mwili wa marehemu tayari umeshafukuliwa
na umeenda kuhifadhiwa katika hospitali ya Wilaya ya Ukerewe kwa ajili
ya uchunguzi na pindi utakapomalizika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani
ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake.
Kwa
upande mwingine, Kamanda Msangi ametoa wito kwa walezi na wazazi kuacha
tabia ya kutoa adhabu za vipigo mara kwa mara kwa watoto pindi
wanapokosea bali wawaelekeze kwa hekima na busara.

No comments