Waziri Mkuu Aweka Jiwe La Msingi Kituo Cha Kupozea Umeme Njia Ya Makambako – Songea
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi kwenye mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 220 kutoka Makambako hadi Songea na kuahidi kuwa Serikali itaendelelea kuwasambazia umeme wananchi wote.
Ametoa ahadi hiyo jana Jumapili, Januari 7, 2018 wakati Akizungumza na wananchi wa eneo la Unangwa nje kidogo ya mji wa Songea, mara bada ya kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa kituo cha kupozea umeme.
Waziri Mkuu alisema ujenzi huo unaenda sambamba na ahadi ya Mheshimiwa Rais, Dk. John Joseph Magufuli ya kuwataka Watanzania wapate umeme kwa urahisi.
“Mheshimiwa Rais ameshusha gharama za umeme kutoka sh. 380,000 hadi sh. 27,000. Zamani ulikuwa unalipia fomu za kuomba umeme, sasa hivi nazo amesema zitolewe bure. Nguzo za umeme zilikuwa zinatozwa sh. 150,000, sasa hivi amesema zitolewe bure,” alisema.
Waziri Mkuu amesema zamani mikoa ya Njombe, Iringa, Ruvuma, Songwe, Mtwara na Lindi ilikuwa na matatizo sufu ya kupata umeme lakini hivi sasa mikoa ya Mbeya na Iringa imepata suluhisho baada ya kukamilika kwa mradi wa umeme wa kilovoti 400 wa kutoka Iringa hadi Shinyanga.
“Sasa hivi tunaingia Njombe na Ruvuma na baadaye tutaenda Mtwara na Lindi,” alisema.
Alitumia fursa hiyo kuwaomba wakazi wanaoishi jirani na mahali kituo hicho kinapojengwa, wawe walinzi wakuu wa mali za mkandarasi ili mradi huo uweze kukamilika mapema.
“Eneo hili lina saruji, nyanya na nondo, si vema watu wachache wjiokeze na kuiba vifaa vya ujenzi. Saidieni kulinda eneo hili, na mali za mkandarasi ili mradi ukamilike kwa wakati,” alisisitiza
No comments