WAMILIKI WA MADINI WATAKIWA KUTUNZA STAKABADHI

Wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wametakiwa kutunza kumbukumbu za matumizi wanayoyafanya kwenye uchimbaji madini ili kujua gharama wanazotumia pindi watakapoanza uzalishaji na Mamlaka ya mapato nchini (TRA) ibaini kiasi cha kodi kinachotakiwa kulipiwa.

Ofisa huduma na elimu wa TRA mkoani Manyara, Joseph Massawe aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wamiliki na mameneja wa migodi ya madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani wilaya Simanjiro, juu ya umuhimu wa ulipaji kodi.

Massawe alisema wamiliki hao wanapaswa kuhifadhi stakabadhi mbalimbali wanazotumia kwenye shughuli zao ili serikali iweze kubaini kiasi wanachotakiwa kulipa tofauti na sasa ambapo wachimbaji wengi hawatunzi kumbukumbu za gharama za uendeshaji wa migodi yao kwa kila siku. 

Alisema wamiliki hao kupitia mameneja na wasimamizi wa migodi ya Tanzanite wanatakiwa kuweka kumbukumbu ya matumizi ya uchimbaji ikiwemo vifaa vya milipuko, malipo ya nishati ya umeme, malipo ya wafanyakazi na matumizi mengine ya kila siku. 

"Endapo watatunza kumbukumbu hizo vizuri itakuwa nafuu kwa wachimbaji hao kwani huenda wanaweza kutumia sh13 bilioni kwa gharama za kuchimba madini hayo na mwisho wa siku wakapata madini ya sh10 bilioni, hiyo itakuwa ni hasara," alisema Massawe.  

Msimamizi wa TRA mji mdogo wa Mirerani, Castory Henry alisema tangu waanze kufanya usajili kwenye kituo hicho October mwaka 2015, waliandikisha wafanyabiashara 300 hadi sasa wamefikia 900 wakiwemo madalali wa madini 130.

Henry alisema wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite 30 wamesajiliwa kulipa kodi kwenye kituo cha Mirerani na wanaendelea na mazungumzo ili kuhakikisha wale wengine wanaolipia kwenye mikoa ya Arusha na Kilimanjaro wanawahamishia katika mkoa wa Manyara. 

"Tumeanza kuwashauri wamiliki wa migodi kuwa, wale wote ambao TIN zao zinasomeka Arusha na Kilimanjaro, wanapaswa kulipia kwenye eneo la kituo cha TRA Mirerani, mahali ambapo wanafanyia uzalishaji wao kupitia madini ya Tanzanite yanayochimbwa kwenye eneo hilo," alisema. 

Hata hivyo, mmoja kati ya wamiliki wa migodi ya Tanzanite, Fatuma Kikuyu aliiomba TRA wawatazame kwa jicho la huruma kwa kutowatoza kodi wanawake wajane wanaochimba madini kama wanavyosamehe kodi kwa taasisi za kidini ikiwemo makanisa na msikiti. 

"Wanawake wajane tunateseka mno kwani tulikuwa na magari na majumba lakini tumeiuza ili kuhudumia migodi ambayo kwa kipindi kirefu haijazalisha chochote, hivyo tumebaki kuombaomba kwenye migodi inayotoa madini, tunaomba TRA watuangalie na sisi kama wanavyoziangalia taasisi za kidini," alisema Kikuyu. 

Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini wa mkoa wa Manyara (Marema) Tawi la Mirerani, Japhari Matambi alisema elimu kama hiyo inayotolewa na TRA inatakiwa mara kwa mara kwa wachimbaji kwani awali walikuwa hawajaelimishwa ipasavyo juu ya ulipaji kodi. 

"Miaka iliyopita viongozi wetu walizoea ujanja ujanja tuu kwa kuangalia maslahi yao, tofauti na sasa ambapo serikali imekuwa inasisitiza ulipaji kodi na sisi kama wachimbaji wa madini tunaunga mkono ulipaji kodi kwa manufaa ya maendeleo ya wananchi wa Tanzania," alisema Matambi. 

No comments