JAMII YATAKIWA KUTOWAFICHA WATOTO WENYE UHITAJI MAALUM
Watoto wenye uhitaji maalum wa shule ya msingi Katesh Wilayani Hanang' Mkoani Manyara, wakiwa na viongozi wa Umoja wa wakuu wakina mama wa shule za sekondari Hanang' (Uwawashuka) waliowapa msaada wa vyakula na vifaa vya kufanya usafi vya thamani ya shilingi milioni moja.
Wazazi na walezi wametakiwa kutokuwafungia ndani walio na watoto wenye uhitaji maalum badala yake wawapeleke shuleni au kwenye vituo maalum ili wakapate elimu kwani nao wana haki ya kusoma kama watoto wengine.
MANYARA
Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake wakuu wa shule za sekondari wilayani Hanang' mkoani Manyara, (Uwawashuka) Esther Malongo aliyasema hayo juzi wakati wakitoa msaada wa vyakula na vifaa vya kufanya usafi vya thamani ya sh1 milioni kwa watoto wenye uhitaji maalum wanaosoma shule ya msingi Katesh.
Amesema kuwa watoto wenye uhitaji maalum wakiwemo wenye ulemavu wa ngozi, macho, mikono, mtindio wa ubongo, viziwi na wengineo wakipatiwa elimu wana uwezo wa kufanya mambo makubwa yatakayonufaisha jamii kwa sasa au miaka ijayo.
Malongo alisema jamii inapaswa kuwapa nafasi watoto wenye uhitaji maalum na siyo kuwatenga, kwani wamefika kwenye kituo hicho cha shule ya msingi Katesh na kujione
a vipaji vingi kwa watoto hao bila kujali mapungufu waliyonayo.
a vipaji vingi kwa watoto hao bila kujali mapungufu waliyonayo.
Alisema umoja wa Uwawashuka wenye wanachama nane umechanga na kuandaa fedha hizo na kuwanunulia zawadi hizo ili kuhamasisha elimu hasa kwa watoto wenye uhitaji maalum katika shule hiyo ya msingi Katesh.
Alisema wanaunga mkono kauli mbiu ya elimu, kazi na nidhamu vitaondoa umaskini Hanang' hivyo watoto hao wenye uhitaji maalum wataweza kubadili mtazamo wa baadhi ya watu pindi wakipatiwa elimu na kufaulu vyema masomo yao.
"Kuwezesha kielimu watoto wenye uhitaji maalum ni jambo zuri mno na tunaiunga mkono serikali kwenye jambo hili kwani lengo la kuwa na Taifa lililoelimika kwa kupata elimu bora litafanikiwa," alisema Malongo.
Katibu wa Uwawashuka, Gisela Msoffe lengo la umoja wao kutoa msaada huo wa sh1 milioni ikiwemo vyakula, vinywaji, vifaa vya kufanyia usafi na mbuzi mmoja ni kuwaonyesha watoto hao wenye uhitaji maalum upendo walio nao kwao.
Msoffe alisema jamii, taasisi na asasi zisizo za serikali nazo zinapaswa kuiga mfano wao kwa kuwajali watu wenye uhitaji maalum kwa kuwapa misaada mbalimbali na siyo kuiachia jukumu hilo serikali peke yake.
"Tunawahamasisha watoto hawa wenye uhitaji maalum kuwa wanaweza na kuwajengea uwezo zaidi ili wafikie malengo ya ufaulu kwa asilimia 100 bila kuwasahau walimu wao wenye moyo wa huruma na kuwajali watoto hawa," alisema.
Mmoja kati ya watoto wenye uhitaji maalum, Adam Hamis ambaye ni mlemavu wa macho anayesoma darasa la tano alisema lengo lake ni kuhakikisha anazingatia masomo ili miaka ya baadaye aweze kuwa profesa.
Hamis alisema anavutiwa na utendaji kazi wa Rais John Magufuli anavyowajali wanyonge kwani mara nyingi anamsikia kwenye redio namna anavyowajali, anavyowatumikia, anavyowatendea haki na kuwathamini watanzania wote bila kuwabagua.

No comments