NINI MAANA YA MAZINGIRA



Mazingira ni vitu vyote vinavyotuzunguka vyenye uhai na visivyo na uhai. Vitu vyenye uhai ni pamoja na mimea na wanyama na visivyo ni pamoja na uhai ni hewa, ardhi na maji

 Mazingira yanahusisha pia vitu vyote vinavyosaidia kuendelea kuwepo kwa maisha ya mwanadamu na viumbe wengine. Hivyo basi maisha ya viumbe hai wa kizazi kilichopo na kijacho kinategemea uwepo wa mausiano mazuri kati ya watu namazingira.

UWEKEZAJI USIOZINGATIA TARATIBU KATIKA KILIMO UNAANGAMIZA MISITU.
UWEKEZAJI katika mashamba makubwa na usiofuata taratibu, unachochea ufyekaji misitu na kuhatarisha ustawi wa misitu nchini, imefahamika.
Hofu hiyo inathibitishwa na yaliyotokea mkoani Lindi katika miaka ya hivi karibuni ambako ardhi iliyochukuliwa kutoka vijiji vinne wilayani Kilwa kwa ajili ya uwekezaji kwenye kilimo cha mibono ilikuwa ya misitu minene ya asili, ikiwa na miti mikubwa yenye thamani.
Wataalamu wa misitu wanaielezea hatua hiyo kutokuwa  rafiki kwa mazingira kwa sababu inachochea kupotea kwa misitu nchini.
Miongoni mwa miti iliyomo kwenye ardhi iliyotolewa kwa ajili ya uwekezaji kwenye kilimo cha mibono, kwa mujibu wa wakazi wa vijiji hivyo, ni pamoja na mninga, mpingo, mkangazi, msekeseke na mkongo.
Mti wa mninga unatajwa kutoa mbao zenye thamani zaidi katika soko la mbao nchini na duniani, kikubwa zikitumika kutengeneza samani. Kwa upande wa mpingo ni mti wenye kutumika na wenyeji wa mikoa ya Lindi na Mtwara kutengeneza vinyago, moja ya sanaa yenye thamani kubwa duniani.
Vijiji vilivyotoa ardhi yao kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo cha mibono wilayani Kilwa ni Mavuji, Migelegele, Liwiti na Nainokwe, vyote vikiwa katika Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi.
Katika kile kinachonekana ulikuwa mkakati maalumu wa kufanikisha kampuni hiyo inapata ardhi hiyo kirahisi, upimaji ulifanyika pale mwekezaji alipofika kukabidhiwa ardhi aliyopewa. Kilichofanywa na vijiji ilikuwa kutenga maeneo tu kwa ajili ya matumizi mbali mbali.
Utafiti wa Shirika lisilo la Kiserikali la Hakiardhi unaonyesha kuwa Kampuni ya Bioshape iliomba hekta 82,000 za ardhi katika Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi. Hata hivyo ilipatiwa hekta 34,000 ambapo walitumia hekta 400 tu za shamba la majaribio.
Mahojiano ya hivi karibuni kati ya waandishi wa habari kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira nchini (JET) waliotembelea vijiji hivyo, yanaibua mkanganyiko kuhusu ukubwa halisi wa eneo lililotolewa na vijiji hivyo kwa kampuni hiyo ya Bioshape.
Wakati tafiti za wataalamu zinaonyesha ni hekta 34,000, serikali za vijiji wanataja takwimu chini ya hizo.
Mathalan, katika Kijiji cha Mavuji, Mjumbe wa Serikali ya Kijiji, Muhidini Ulambe anasema walitoka ekari 16,000 ambazo ni chini ya hekta 10,000. Eneo hilo awali lilikuwa ni msitu wa asili.
Afisa Mtendaji Kijiji cha Naikone, Abdallah Said Kigomba anasema wao walitoa ekari 16,000.89 nazo zikiwa chini ya hekta 10,000.
Pamoja na ekari 16,000 ambazo Kijiji cha Mavuji wanaeleza kutoa, pia kijiji hicho kilitoa hekta zake 1,000 kutumika na mwekezaji kama shamba la mfano.
Wananchi wafichwa mikataba
Katika hali yenye kutia shaka, hakuna hata kijiji kimoja chenye nakala ya  mkataba wenywe kuonyesha ardhi waliyoitoa kwa mwekezaji huyo. Kilichopo kwenye vijiji hivyo ni mkataba wa ahadi za mwekezaji kwa vijiji.
Sheria ya ardhi inaweka ukomo wa kiwango cha utoaji ardhi kwa kila ngazi ya uongozi ambapo kwa kijiji mwisho ni hekta 50, zaidi ya hapo hutolewa kwa idhini ya Rais baada ya wanakijiji kuridhia iwapo eneo wanalo.
Kilichofanyika kwa ardhi iliyochukuliwa kwenye vijiji hivyo vinne wilayani Kilwa, ni maafisa wa Serikali kuwashawishi wananchi kuwakubalia wawekezaji kuchukua eneo wanalolihitaji na wakaridhia wakiwa hawaelewi wanaridhia kuchukuliwa ardhi ya ukubwa gani.
Nakala za mikataba hiyo zinaonyesha kuwa mikataba iliandaliwa na Kampuni ya uwakili ya FK Law Chambers, Advocates na Kitengo cha sheria, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi. Vijiji vilipelekewa na viongozi wake kutakiwa kusaini tu.
“Tuliletewa mkataba kusaini tu, kati yetu na mwekezaji kuhusu masharti tuliyowapa, mkataba ulitengezwa na mwekezaji na halmashauri,” anasema Yusuf Mohamed, maarufu kama Tangi.
Tangi ndiye  aliyekuwepo wakati wa utoaji wa ardhi hiyo kwa mwekeji huyo wa ajili ya kilimo cha mibono akiwa kama mwenyekiti wa Kijiji.
Afisa Programu kutoka taasisi isiyo ya kiserikali ya HAKIARDHI, Joseph Chiombola, anaubainisha udhaifu huo kuwa unachangiwa zaidi na utaratibu wa wananchi au vijiji kusaini nyaraka kwa msukumo wa kupata pesa au ahadi.
“Tatizo la wananchi wengi ni kukubali kusaini nyaraka za fidia bila kusoma na kuelewa kilichomo kwenye nyaraka hizo,” anasema Chiombola ambaye kitaaluma ni mwanasheria.
Kiombola aliibainisha changamoto hiyo wakati akitoa mada kuhusu umiliki wa ardhi nchini kwa waandishi wa habari walio katika Mpango wa Ardhi yetu Ajenda Yetu unaotekelezwa katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Pwani na Lindi na kuratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET).
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo kwenye tovuti ya  https://www.tnrf.org/, Kampuni ya Bioshape Tanzania ambayo ni uzao wa Bioshape Holdings ya nchini Uholanzi, ilianzishwa nchini kwa ajili ya kilimo cha mashamba makubwa ya mibono.
Hata hiyo, kampuni hiyo haikuwekeza kwenye kilimo hicho kama walivyoahidi kwa vijiji hivyo pamoja na Serikali.
Wavuna miti wakatelekeza mibono
Kijiji pekee walichoanzisha shughuli zao kati ya vinne walikopewa ardhi, ni Majivu ambako waliandaa vitalu vya mibono ambavyo hata hivyo inaelezwa kuwa walivitelekeza na hawakuwahi kuvuna.
Katika vijiji vilivyobakia, mwekezaji hakuwahi kufanya jambo lolote, ardhi aliyopewa ilibaki vile vile, wakati katika Kijiji cha Majivu walivuna miti yote mikubwa kwenye eneo walilopewa na kuliacha likiwa na miti midogo na vichaka tu.
Mmoja wa wafanyakazi wa Kampuni hiyo, Jafari Mbudo anathibitisha mwekezaji huyo kuandaa vitalu kwenye shamba la mfano, lakini wakijihusisha zaidi na uvunaji mazao ya misitu.
“Dhumuni walilotueleza ilikuwa kulima mibono, walipanda katika shamba la mfano, lakini hawakuwahi kuvuna, kikubwa nilichokiona, walivuna miti na kupasua mbao, wakapakia kwenye containers,”  anasema Mbudo.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mpingo Conservation and Development Initiative, Makala Jasper anasema shirika lao lilikuwa la kwanza kupiga kelele wakitoa tahadhari kuhusu kutoa maeneo ya misitu kwa ajili ya uwekeaji.
“Uwekezaji unaofyeka misitu na usiofata taratibu haufai, unaangamiza misitu,” anasema Jasper.
Shirika hilo lilishuku hadi Tathmini ya mazingira (EIA), kwamba ilikuwa ya kugushi na taratibu hazikufuatwa.
Jasper anabainisha kuwa iwapo EIA ingefanyika vizuri, ingebainika tokea mwanzo kuwa uwekezaji wao haukuwa wa manufaa.
Uwekezaji kwenye uvunaji mazao ya misitu ulikuwa mkubwa zaidi ikilinganishwa na kilimo chenyewe cha mibono ambayo ndiyo shughuli yao ya msingi (core business).
“Nguvu waliyoitumia kwenye kuvuna mazao ya misitu na waliyotumia kwenye kilimo cha mibono vilikuwa haviwiani,” anasema Jasper.
Baadhi ya wanavijiji walioajiriwa kwenye kampuni hiyo, wanafichua kuwa mwekezaji aliwekeza mitambo mikubwa ya kuvunia miti na kupasua mbao, wakati kwenye zao la mibono, vitalu vyake ni kama watu walikuwa wanacheza, hakukuwa na umakini wowote.

No comments