Godliver Gordian Avunja Ukimya: “Ni Kweli Ndoa imenishinda, nikaamua Kujiondoa”.

Mwigizaji mahiri wa filamu nchini Tanzania, Godliver Gordian, hatimaye amethibitisha uvumi uliokuwepo kwa muda mrefu kuhusu maisha yake ya ndoa. Kupitia mahojiano yake, Godliver amekiri wazi kuwa ndoa yake imevunjika, na ameamua kuachana na Mumewe baada ya kuona mambo hayaendi kama alivyo tarajia.

"Ni kweli sipo kwenye ndoa. Ndoa sio jambo dogo kabisa, niliona imenishinda nikaona ya nini nikajiweka pembeni,"* amesema Godliver kwa ujasiri.

Godliver na mumewe walifunga ndoa mwaka 2023, lakini kufikia mwaka 2024 tetesi zilianza kusambaa kuwa wawili hao hawako tena pamoja, ingawa hakukuwa na tamko rasmi kutoka kwa upande wake hadi sasa.

Kwa muda mrefu, mashabiki wake walikuwa wakijiuliza kuhusu hali ya ndoa yake, hasa baada ya mabadiliko kadhaa kuonekana katika maisha yake ya mitandaoni. Hatimaye, sasa ameweka wazi hali halisi, na kuonesha kuwa alichukua uamuzi huo kwa kujilinda na kujiheshimu.

“Sikuchukua uamuzi huo kwa hasira au chuki, ila ni kwa sababu niliona haifanyi tena kazi kwangu. Nikaamua nijitazame mimi na maisha yangu," aliongeza.

Hatua hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti na mashabiki wake, wengine wakimpongeza kwa ujasiri wake wa kukiri ukweli bila aibu, huku wakimtakia nguvu mpya katika safari yake ya maisha.

Katika jamii inayoweka shinikizo kubwa kwa Wanawake kubaki kwenye ndoa kwa gharama yoyote, uamuzi wa Godliver unafungua mjadala mpana kuhusu uhuru wa Mwanamke kujiondoa katika mazingira yasiyo na afya.

Kwa sasa, Godliver ameweka mkazo zaidi kwenye kazi zake za sanaa na ameendelea kuwa mfano wa mwanamke jasiri anayejiamini na kujisimamia katika maamuzi yake.


No comments