SIJIPENDEKEZI NA SIO OMBAOMBA KWA HALMASHAURI"- RC MAKONDA
"SIJIPENDEKEZI NA SIO OMBAOMBA KWA HALMASHAURI"- RC MAKONDA
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amekiomba Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha kumpa ushirikiano katika kuwaletea maendeleo wakazi wa Arusha kwa kufichua uzembe na udhaifu wa kiutendaji katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020/2025.
Kauli ya Mhe. Paul Christian Makonda ameitoa leo Mei 30, 2024 wakati wa muendelezo ya ziara yake ya kikazi kwenye Wilaya zote za Mkoa wa Arusha ambapo amepita kwenye Ofisi za CCM Wilaya ya Arusha ili kusalimia na kujitambulisha kwao kabla ya kuanza ziara kwenye Wilaya hiyo.
Mhe. Mkuu wa Mkoa amekiambia Chama Cha Mapinduzi kuwa amedhamiria kikamilifu kupambana na wazembe, wabadhirifu na wala Rushwa akikemea kuendekezwa kwa siasa na ujuaji kunakofanywa na watumishi na watendaji wa Ngazi mbalimbali ndani ya Mkoa badala ya kuwatumikia wananchi.
Mhe. Makonda kadhalika amewataka wakuu wa idara, wakuu wa Wilaya na maofisa wa Chama Cha Mapinduzi kutoendekeza madai ya posho na fedha kutoka kwa wakurugenzi na wahasibu wa Halmashauri zao akieleza kuwa suala hilo linafifisha nguvu na uwezo wa kuweza kuwasimamia watendaji waliochini yao.
Aidha Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Christian Makonda amesema hana haja ya kujipendekeza na badala yake ameelekeza utumishi wake kwenye kuwatumikia wananchi wa Arusha ili kuweka alama na maana katika maisha yao kwa kuwaondolea changamoto na kero mbalimbali zinazowasibu.
Awali Uongozi wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Arusha pamoja na idara zake zote walipata nafasi ya kusali pamoja na Mhe. Makonda na kumuombea kwa Mwenyenzi Mungu amuongoze na kumjalia kheri katika kuwatumikia wana Arusha.
No comments