MOTO WA RC MAKONDA KUHAMIA MONDULI.
MOTO WA RC MAKONDA KUHAMIA MONDULI.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda Kesho Mei 27, 2024 anatarajia kuendelea na ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi na kutatua kero za wakazi wa Monduli Mkoani Arusha.
Kesho itakuwa ni muendelezo wa ziara ya Mkuu wa Mkoa ya kutembelea wilaya zote za Mkoa wa Arusha, ambapo ziara hiyo tayari imefanyika kwa matokeo makubwa kwenye wilaya za Longido na Karatu ilipofanyika Ijumaa ya Mei 24, 2024.
Akiwa Wilayani Longido na Karatu, Mhe. Makonda alikagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule ya Sayansi ya wasichana Samia Longido na mradi wa ujenzi wa ofisi za makao makuu ya Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro yanayojengwa Wilayani Karatu kando ya miradi mingine mingi inayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhe Mkuu wa Mkoa pia alipata nafasi ya kuzungumza na watendaji wa Wilaya za Longido na Karatu, msisitizo wake Mkubwa ukiwa ni kuwataka watendaji na watumishi wa ngazi za wilaya na kata kuhakikisha kuwa wanawatumikia wananchi kikamilifu katika kuwaharakishia maendeleo na kutimiza ahadi za serikali na ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020-2025.
Aidha Mhe. Mkuu wa Mkoa pia amefanya mikutano ya hadhara kwenye wilaya za Longido na Karatu ambapo kero zaidi ya 200 zilisikilizwa, kutatuliwa na nyingine kutolewa maelekezo ya kiutendaji kwa mamlaka na idara mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Christian Makonda kwa usaidizi kutoka kwa Mawakili wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) mkoa wa Arusha walitoa pia usaidizi wa kisheria kwa wananchi mbalimbali waliokuwa wanakabiliwa na mashauri yenye kutaka tafsiri ya Kisheria na ushauri wa Kisheria.
Kwenye ziara hiyo Mkuu wa Mkoa amekuwa akitumia magari maalum ya kubebea watalii mkoani hapa kama sehemu ya jitihada zake za kuhamasisha na kukuza uelewa kuhusu utalii na fursa zake pamoja na kufungamanisha maisha ya wananchi wa Arusha na utalii uliopo mkoani Arusha ili kuweza kuwa mabalozi wa utalii na walinzi wa amani ikiwa ndiyo silaha kuu ya kuendelea kuvutia wageni kufika mkoani Arusha kwa shughuli mbalimbali za kitalii, mikutano, michezo pamoja na Biashara.
Akiwa Monduli Jumatatu hii Mhe. Mkuu wa Mkoa atatembelea na kukagua miradi mbalimbali ya Maendeleo inayotekelezwa wilayani Monduli kabla ya jioni kufanya Mkutano wa hadhara wa kuwasikiliza na kutatua kero za wananchi wa wilayani Monduli.
No comments