WAZAZI SHIRIKISHANENI MAANDALIZI YA UTUNGAJI MIMBA


WAZAZI nchini wametakiwa kujenga utamaduni wa kukaa pamoja na kushirikishana  maandalio ya utungaji mimba kwa ajili ya mama kupata mtoto ndani ya familia.

Wito huo ulitolewa jana wilayani Monduli kwenye mafunzo ya Uhudumu wa afya katika jamii kuhusiana na huduma jumuishi za afya ya mama, mtoto mchanga na mtoto chini ya miaka mitano.

Mafunzo hayo yalitolewa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la World Vision Tanzania kupitia mradi wake wa Kisongo Makuyuni yalishirikisha watoa huduma 26 wa ngazi ya kijiji.

Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo Mganga wa wilaya ya Monduli Dk. Titus Mmasi aliwataka wahudumu hao wa afya ngazi ya jamii kutumia mafunzo waliyopewa ili kuisaidia jamii ya kifugaji katika kuelewa umuhimu wa afya ya uzazi.

“Afya ya uzazi wa mpango haijazungumzwa kwa uwazi katika ngazi ya familia, ni utamaduni mgumu kwetu. Baba na mama huwa mnafanya maandalio ya kukaa na kupanga mwezi upi muanze kutafuta mtoto?

“Ujauzito wa wengi hutokea bahati mbaya, hili jambo tunatakiwa kwenda kufundisha unaweza kukosa sababu za kumlaumu mjamzito aliyekuja na mimba ya miezi mitano kutokana na kusema pale alipojiskia ana ujauzito.

“Kwa kuwa mmepata elimu sasas nendeni mkawaelimisha kuwa tendo la kupata mtoto ni la kupanga mipango, waambie dalili zake ni zipi baada ya mimba kutungwa ataanza kusubiria hizo dalili kwa kuwa alipata elimu.

“Ukimuachia bila kumpa elimu ya tendo la kutafuta mtoto anaweza kuendelea kuishi akisubiria mtoto aje na mwisho wa siku atakuja na miezi mitano akiwa hajagusa kidonge cha kuongeza damu,kuzuia magonjwa ya kuzaliwa kama kichwa kikubwa,  mgongo wazi na midomo Sungura,” alisema Dk. Mmasi.

“Tukawashawishi tukiweza kumaliza maboma yetu na kila mtu akatimiza wajibu wake tutakuwa na jamii yenye afya bora zaidi kwani bado kuna watu hawajafikiwa na elimu ya afya na uzazi wa mpango,” alisema.

Akielezea suala la mila katika jamii hiyo ya Kimaasai Dk. Mmasi alisema jambo hilo limekuwa likikwamisha utumiaji wa vyakula vinavyorutubisha afya ya mama mjamzito na mtoto.

“Suala la lishe ya mama, mtoto na jamii yetu tunatakiwa kulitilia mkazo, badala ya kula mara mbili kwa siku ni tukawafundisheni kuwalisha watoto mara tatu kwa siku ili kuwapusha na magonjwa ya Kwashakoo na Utapiamlo,”alisema Dk. Mmasi.

Kwa upande wake Mratibu wa Shirika la World Vision Tanzania Kanda ya Babati anayeshulikia afya na lishe Joan Msuya alisema, mradi huo umelenga eneo la afya ya mama na mtoto kutokana na kuwapo kwa udumavu na utamlo kwa watoto kwenye maeneo ya umasaini.

Aliitaja changamoto nyingine iliyopo kwenye maeneo hayo alisema ni pamoja na wanawake wajawazito kujifungulia majumbani, kutohudhuria Kliniki na watoto kutopatiwa chanjo.

“Tumeendesha mafunzo haya kwa watoa huduma ngazi ya jamii katika mradi wa Kisongo-Makuyuni. Hawa ni miongoni mwa wanaokutana na jamii na kuihamasisha iende Zahanati, kupata chanjo na kutumia uzazi wa mpango.

“Sisi World Vision Tanzania malengo yetu ni kuona mtoto akifurahia maisha kwa ujumla wake unaohusisha elimu, afya, lishe na maendeleo,” alisema Msuya.

Naye Afisa Afya wilaya ya Monduli Jubilate Temu akizungumza afya ya usafi pamoja choo aliwataka watoa huduma hao kuhakikisha wanakwenda kuhamasisha kampeni ya uchimbaji wa vyoo.

“Katika wilaya yetu tatizo la uwapo vyoo bado ni kubwa jamii ya kifugaji imekuwa na mazoea ya kutumia mapori na vichaka. Ndugu zangu kwa sasa tupo kwenye mapambano kila nyumba lazima iwe na choo,” alisema Temu na kuongeza:

“Hakuna tena suala la kujisaidia hovyo kwenye vichaka, chukueni jukumu hili kwa pamoja kuhakikisha kila kaya inapata choo hii ni kampeni ya kitaifa,” alisema.

Aidha mshiriki wa mafunzo hayo Grace Ndemfoo alisema mafunzo hayo yaliyolenga afya ya mama na mtoto katika jamii yamewapa mwanga zaidi wa kuisaidia jamii wanayoishi nayo.

“Katika mafunzo yetu tumembelea kaya 46 na wakati wa mafunzo yetu tulikutana na mama mjamzito akiwa na upungufu wa damu tulimhudumia na anaendelea vizuri,” alisema Ndemfoo.

Mratibu wa Shirika la World Vision Tanzania Kanda ya Babati anayeshulikia afya na lishe Joan Msuya
Mganga wa wilaya ya Monduli Dk. Titus Mmasi ,akimkabidhi cheti mwananchi kutoka wilayani hapo.




Mwisho.

No comments