IFAHAMU HISTORIA YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

Watanzania wametungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Wanawake.

Kwa kawaida siku hii ambayo huadhimishwa kila mwaka, hapa nchini huwezesha wanawake kukutana kwa kuanzia na maandamano. Maandamano hutawaliwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali wa kuhamasisha maendeleo ya mwanamke. Siku hiyo hutolewa mada na hotuba mbalimbali zinazomhusu mwanamke na maendeleo yake. Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotoa kipaumbele kwa maadhimisho haya.

Kihistoria, siku hiyo ilianza kwanza kwa kuitwa siku ya wafanyakazi wanawake ya kimataifa na ilikuwa inaadhimishwa kila Machi 8. Lengo la maadhimisho lilikuwa ni kumuonesha upendo na heshima mwanamke kutokana na mafanikio yake katika nyanja mbalimbali kama vile siasa, kijamii na kiuchumi. Ni siku ambayo wanawake hutambuliwa kutokana na mafanikio yao bila kujali mgawanyiko wa taifa, kabila, lugha, itikadi, kitamaduni, kiuchumi au kisiasa.

Hukumbusha jitihada za nyuma na mafanikio, na muhimu zaidi, kwa ajili ya kuangalia mbele kutokana na uwezo wa wanawake waliopita kwa ajili ya kujenga zaidi kizazi kijacho. Maadhimisho rasmi ya siku hiyo muhimu kwa wanawake, yalianza Machi 8, 1857 baada ya wafanyakazi katika kiwanda cha nguo jijini New York nchini Marekani kugoma kutokana na mazingira mabaya waliyokuwa wakikabiliana nayo katika kiwanda hicho.

Kutokana na mgomo huo, uongozi wa kiwanda ulichukua hatua ya kudhibiti mgomo huo kwa njia ya ukatili na dhuluma kwa kuwafungia katika chumba kimoja cha jengo hilo wanawake wote waliokuwa wakifanyakazi . Bila kujali wala kuonesha huruma kwa wanawake hao, waliteketeza jumba hilo na inakadiriwa kuwa takribani wanawake 129 walipoteza maisha yao kutokana na moto huo.

Tukio hilo liliibua hisia kali duniani kote na maelfu ya raia walihudhuria mazishi ya wanawake hao hali iliyolifanya tukio hilo kuwekwa kwenye vitabu vya historia zitakazoendelea kukumbukwa duniani. Mwaka 1910, nchini Denmark kulifanyika kongamano kubwa kwa ajili ya kuwakumbuka wanawake hao waliofariki na azimio lilipitishwa kuwa Machi 8 ya kila mwaka, ifanyike siku ya Wanawake Duniani kwa ajili ya kuwakumbuka wanawake hao lakini pia kuamsha hamasa ya maendeleo kwa wanawake wote.

Pamoja na kwamba siku hiyo ilipingwa vikali na mataifa mengi duniani, kupitia Umoja wa Mataifa (UN), siku hiyo ilianza kuadhimishwa rasmi mwaka 1975. Miaka miwili baadaye, Desemba mwaka 1977, Baraza Kuu la UN lilipitisha na kutangaza kuadhimisha Siku ya Haki za Wanawake na Amani ya Kimataifa. Tangu kuanza kuadhimishwa kwa siku hiyo ya wanawake duniani, imekuwa na mwelekeo mpya wa kimataifa, kwa ajili ya wanawake katika nchi zote zilizoendelea na zinazoendelea.

UN imekuwa ikisaidia kujenga urithi wa kihistoria wa kimataifa kukubali mikakati na viwango vya mipango na malengo ya kuendeleza hali ya wanawake duniani. Umoja huo na mashirika yake umekuza ushiriki wa wanawake kama washirika sawa na wanaume katika kuleta maendeleo endelevu, amani, usalama, na heshima kwa ajili ya haki za binadamu. Kwa Tanzania maadhimisho hayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka lakini kuanzia mwaka 2005 Serikali ilipitisha uamuzi kuwa, yafanyike kitaifa kila baada ya miaka mitano.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Sihaba Nkinga, uamuzi huo, umelenga kutoa muda wa utekelezaji wa maazimio na kupima mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitano. Nkinga anasema maadhimisho hayo hutoa fursa kwa Serikali, wananchi, wadau, na wanawake wenyewe kupima utekelezaji wa maazimio, matamko na mikataba ya kimataifa, kikanda na kitaifa inayohusu masuala ya maendeleo ya wanawake na usawa wa jinsia.

“Siku ya wanawake duniani husisitiza kujenga mshikamano wa wanawake wote duniani, kuhamasisha jamii kutafakari kaulimbiu ya maadhimisho hayo kila mwaka; kuelimisha jamii kuhusu jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali na asasi mbalimbali yakiwemo Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika kuwaendeleza wanawake; na kuhamasisha jamii kuhusu utekelezaji wa sera na mipango mbalimbali ya serikali yenye lengo la kudumisha amani, usawa na maendeleo,” anasema Nkinga.

Kimsingi Tanzania imepiga hatua tangu kuanza kuadhimisha siku ya wanawake duniani, kwani kumekuwa na mwamko mkubwa wa wanawake kushiriki katika maendeleo na ngazi za uamuzi ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Ukweli ni kwamba, awali wanawake wengi walikuwa wakihofia hata kuwania nafasi kubwa za kisiasa kama vile urais, ubunge na nafasi nyingine za kiutendaji kutokana na hofu ya kutopewa nafasi.

Kwa mfano kwa miaka zaidi ya 40, ushiriki wa wanawake bungeni ulikuwa haufiki asilimia 20. Taarifa zinaonesha kuanzia mwaka 1961 hadi 1965 ushiriki wa wanawake bungeni ulikuwa ni asilimia 1.9 wakati wanaume ilikuwa asilimia 98.1. Mwaka 1965 hadi 1970 wanawake ushiriki wao ulikuwa asilimia 4.0 wakati wanaume, mwaka 1970 hadi 1975 asilimia 4.0, mwaka 1975 hadi 1980 asilimia7.3, mwaka 1980 hadi 1985 asilimia 10, 1985 hadi 1990 asilimia 10 na mwaka 1990 hadi 1995 asilimia 18.

Hivi sasa kutokana na harakati mbalimbali ikiwemo mikakati inayowekwa katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, hali imebadilika na idadi ya ushiriki wa wanawake katika chombo hicho kwa sasa inafikia takribani asilimia 22. Hata vinyang’anyiro vya nafasi za juu za uongozi, wanawake wameanza kujitokeza kuwania. Mwaka 2005, ndipo mwanamke wa kwanza aliandika historia ya kuwania urais. Alikuwa Dk Anna Senkoro (sasa marehemu) aliwania kupitia chama cha PPT-Maendeleo.

Baada ya hapo, wanawake wengine waliojitokeza ni Anna Mghwira wa ACT-Maendeleo aliyeingia kwenye kinyang’anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Wanawake wengine waliowania nafasi hiyo katika ngazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni Asha- Rose Migiro na Amina Said.

Wakati huo huo historia imeandikwa nchini kutokana na nafasi ya Makamu wa Rais kushikwa na mwanamke, Samia Suluhu Hassan. Wakati Tanzania ikiendelea kupigania haki ya mwanamke kupitia maadhimisho haya, mwaka huu, yataongozwa na kauli mbiu inayosema Tanzania ya Viwanda: Wanawake ni Msingi wa Mabadiliko ya Kiuchumi

No comments