Serikali Kupunguza Vifo vya Watoto Wachanga



Serikali  imesema itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika  kupunguza vifo vya watoto wachanga ili kufikia malengo ya mpango mkakati wa mwaka 2030.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Dkt. Mariam Kalomo kutoka Wizara ya Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto alipokua akizungumza katika hafla ya kupokea msaada wa vifaa tiba kutoka Taasisi ya Vodacom ambavyo vimetolewa kwa ajili ya watoto wachanga ambao wamezaliwa kabla ya wakati  katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Dkt. Kalomo ambaye amemuwakilisha Naibu Waziri wa Afya Dkt . Faustine Ndugulile amesema mikakati ya kupunguza vifo vya watoto wachanga haiwezi kuwa endelevu bila kushirikiana na wadau wa sekta ya afya pamoja na wadau wa sekta binafsi.

‘‘Nichukuke fursa hii kuwapongeza na kuwashukuru Vodacom Foundation kwa kuona umuhimu na uhitaji wa kuwasaida watoto wachanga kwani msaada huu sio tu utarahisisha utendaji wa wahudumu wetu lakini pia utasaidia kuokoa maisha ya watoto wachanga na watoto wanaozaliwa kabla ya muda.’’amesema Dkt. Kalomo.

Awali akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Prof. Lawrence Museru, Kaimu Mkurugenzi wa Uuuguzi na Ukunga MNH, Sista Zuhura Mawona  amesema takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania imejitahidi kupunguza vifo vya watoto kulinganisha na makubaliano  yaliyowekwa kimataifa.

 ‘’Kwa mujibu wa  takwimu za mwaka 2015 vifo vya watoto wachanga viko katika kiwango cha 18.8-21/1000 kati ya watoto walio hai,  vifo vya watoto wachanga vinachangia kiwango cha asilimia 40 katika takwimu za vifo vya watoto wote walioko chini ya miaka mitano’’ amefafanua Sista Zuhura.

Akisisitiza amesema katika Kitengo  cha watoto wachanga  Muhimbili, vifo vya watoto hao vipo katika asilimia 18.8 hivyo imelazimu kutafuta mikakati ya kupambana na tatizo hilo.

Amesema MNH imedhamiria kuendelea kutoa huduma  kwa uadilifu ambapo  imeanzisha mfumo wa uongozi ambao umetengeneza muongozo wa kuboresha utendaji  mara kwa mara, pia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili inafanya kazi kwa ushirikiano na serikali pamoja na wadau wengine katika kuhakikisha inatoa huduma bora kwa watoto wachanga.

Kupitia ushirikiano huo  Muhimbili  imeboresha kitengo cha watoto wachanga pamoja na kujenga wodi za uangalizi maalumu ambayo itaweza kupokea  watoto 15 kwa  wakati mmoja, hii ni pamoja na kuwepo kwa vifaa vyenye ufanisi mkubwa kama mashine za kusaidia katika upumuaji- (CPAP).

Vifaa  vilivyotolewa ni mashine za kuvuna hewa ya oxygen-2, mashine za kutoa unyevunyevu, mashine 5  za kuwezesha upumuaji –CPAP, mashine 5 za kulishia na kuwekea dawa, dawa 10 za kukomaza mapafu, nepi za watoto pakiti 50 na  kanga pea  50. Vifaa hivyo vitasaidia kuongeza ufanisi  katika matibabu ya watoto wachanga  ambao wamezaliwa kabla ya wakati .

  Dkt. Mariam Kalomo kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto akipokea misaada mbalimbali ikiwamo vifaa tiba pamoja na kanga kutoka Vodacom Foundation kwa niaba ya Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Faustine Ndugulile. Misaada hiyo imetolewa kwa ajili ya kuwasaidia watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambao wanazaliwa kabla ya wakati.
 Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Sister Zuhura Mawona ambaye amemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru akizungumza kabla ya misaada hiyo kukabidhiwa katika hospitali hiyo leo.  
 Baadhi ya wafanyakazi wa Vodacom wakiwa kwenye hafla hiyo leo.
  Daktari Bingwa wa Watoto, Dkt. Martha Mkonyi akitoa maelezo kuhusu matumizi ya vifaa tiba katika hafla hiyo.
 Dkt. Mariam Kalomo kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Muhimbili pamoja na Vodacom

No comments