Janga la tabianchi: mambo 5 ya kuzingatia 2025
Janga la tabianchi: mambo 5 ya kuzingatia 2025

Mwanafunzi nchini Viet Nam akitoa mbegu
Mji wa Amazon wa Belém, Brazili, utakuwa kitovu cha juhudi za kimataifa za kukabiliana na janga la mabadiliko ya tabianchi mwezi Novemba 2025, wakati utakapoandaa moja ya mikutano muhimu ya Umoja wa Mataifa ya mabadiliko ya tabianchi hivi karibuni.
Hadi wakati huo, kutakuwa na fursa nyingi za kufanya maendeleo makubwa katika masuala kadhaa yanayohusiana na tabianchi, kuanzia kwenye viwango vya kushangaza vya uchafuzi wa plastiki hadi kufadhili mpito wa kuhamia uchumi wa kimataifa unaojali mazingira.
1. Je, tunaweza kuhakikisha lengo la nyuzi joto 1.5 linakuwa hai?
"Kuhakikisha lengo la nyuzijto 1.5 linakuwa hai" imekuwa kilio cha hadhara cha Umoja wa Mataifa kwa miaka kadhaa, ikimaanisha lengo la kuhakikisha kuwa wastani wa joto duniani hauzidi nyuzi joto 1.5 zaidi ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda. Makubaliano ya kisayansi ni kwamba kutochukua hatua kutakuwa na matokeo ya janga, haswa kwa mataifa yanayoitwa "mstari wa mbele", kama vile mataifa yanayoendelea ya visiwa ambayo yanaweza kutoweka chini ya bahari huku viwango vya bahari vikiongezeka.

Mwanaume anavua samaki akiwa ameketi katika viroba vya mchanga vinavyokinga kisiwa cha Pasifiki cha Vanuatu
Katika COP30, mkutano wa mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa uliopangwa kufanyika kuanzia tarehe 10 hadi 21 Novemba 2025, upunguzaji yaani, hatua na sera za kupunguza utoaji wa gesi chafuzi zinazochangia kuongezeka kwa joto unatarajiwa kuwa lengo kuu.
Mataifa kote duniani yatawasili yakiwa na ahadi dhabiti na zenye malengo makubwa zaidi ya kupunguza gesi joto. Hii yote ni utambuzi kwamba ahadi zilizopo hazitoshelezi kabisa kukabili viwango vya joto, na ni sehemu ya makubaliano ambayo nchi wanachama zilitia saini mwaka wa 2015 katika Mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi COP, mataifa yanapaswa "kuongeza ahadi zao kila baada ya miaka mitano. Mara ya mwisho hii ilifanyika ilikuwa ni mjini Glasgow kwenye mkutano wa COP mwaka 2021, ambayo ilicheleweshwa kwa mwaka mzima kutokana na janga la COVID-19.
2. Kulinda asili
Kufanya COP30 katika eneo la msitu wa mvua wa Amazon huko Brazili ni muhimu sana. Inakumbusha juhudi za kwanza za kimataifa za kulinda mazingira: "Mkutano wa Dunia", ambao ulisababisha maendeleo ya kuwepo mikataba mitatu ya mazingira juu ya mabadiliko yatabianchi, bayoanuwai na kuenea kwa jangwa, ulifanyika katika jiji la Brazil la Rio de Janeiro mwaka 1992.

Kasuku akiwa ameketi katika tawi la mti Maharashtra, India
Eneo hilo la msitu wa mvua pia linaonyesha jukumu ambalo asili inachukua katika janga la tabianchi. Msitu wa mvua ni "beseni kubwa la hewa ukaa," mfumo ambao unachukua na kuhifadhi gesi chafuzi ya ukaa au CO2 na kuizuia kuingia kwenye angahewa, ambako inachangia ongezeko la joto duniani.
Kwa bahati mbaya, misitu ya mvua na "suluhu zingine za asili" ziko chini ya tishio kubwa kutoka kwenye maendeleo ya binadamu, kama vile ukataji miti haramu ambao umeharibu maeneo makubwa ya eneo hilo. Umoja wa Mataifa utaendelea na juhudi zake za kuboresha ulinzi wa misitu ya mvua na mifumo mingine ya ikolojia mwaka 2024, wakati mazungumzo ya bayoanuwai yatakapoanza tena mjini Roma mwezi Februari.
3. Nani atalipia gharama?
Fedha kwa muda mrefu imekuwa suala mwiba katika mazungumzo ya kimataifa ya tabianchi. Nchi zinazoendelea zinahoji kuwa nchi tajiri zinapaswa kuchangia zaidi katika miradi na mipango ambayo itawawezesha kuondokana na nishati ya mafuta kisukuku na kuimarisha uchumi wao kwa vyanzo vya nishati safi.
Nchi tajiri, kwa upande wao, zinahoji kwamba uchumi unaokua kwa kasi kama vile Uchina, ambayo sasa ni mtoaji mkubwa zaidi wa gesi chafuzi duniani, inapaswa pia kulipa sehemu yao.

Wanaharakati wakiandamana kupinga mafuta kisuskuku kwenye COP29 Baku, Azerbaijan
Mafanikio makubwa yalifanywa katika mkutano wa COP29 huko Baku, Azerbaijan, ikiwa ni pamoja na kupitishwa kwa makubaliano ya kuongeza mara tatu fedha za mabadiliko ya tabianchi zinazoingia katika nchi zinazoendelea hadi dola bilioni 300 kwa mwaka ifikapo 2035. Mpango huo ni hatua ya kusonga mbele, lakini jumla ya mwisho iko mbali kwani kuna ungufu wa dola trilioni 1.3 ambazo wataalam wa tabianchi wanasema zinahitajika kwa nchi zinazoendelea kukabiliana na jnga hilo.
Maendeleo zaidi kuhusu fedha yanaweza kutarajiwa katika mwaka huu wa 2025, katika mkutano wa kilele nchini Hispania mwishoni mwa Juni. Mikutano ya ufadhili wa maendeleo hufanyika mara moja kila baada ya miaka 10, na tukio la mwaka ujao linatajwa kama fursa ya kufanya mabadiliko makubwa kwenye usanifu wa fedha wa kimataifa. Masuala ya mazingira na tabianchi yatatolewa, na suluhu zinayoweza kutokea kama vile ushuru wa kijani, bei ya hewa ukaa na ruzuku zote zitakuwa mezani.
4. Kuweka sheria
Wakati Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ ilipoelekeza umakini wake katika mabadiliko ya tabianchi mwezi Desemba, ilisifiwa kama wakati wa kihistoria kwa wajibu wa kisheria wa mataifa chini ya sheria za kimataifa.

Vanuatu mara nyingi inakabiliwa na majanga ya tabianchi kama typhoons
Vanuatu, taifa la kisiwa katika Bahari ya Pasifiki lililo hatarini zaidi na janga la mabadiliko ya tabianchi limeiomba mahakama ya ICJ kutoa maoni ya ushauri, kufafanua majukumu ya nchi juu ya mabadiliko ya tabianchi na kufahamisha madai yoyote yajayo.
Kwa muda wa wiki mbili, nchi 96 na mashirika 11 ya kikanda yalishiriki katika vikao vya hadhara mbele ya Mahakama, kutia ndani Vanuatu na kundi la mataifa mengine ya visiwa vya Pasifiki, pamoja na mataifa makubwa ya kiuchumi kama vile China na Marekani.
ICJ itafanya mashauri kwa miezi kadhaa kabla ya kutoa maoni yake ya ushauri kuhusu suala hilo. Ingawa maoni hayo hayalazimishi, yanatarajiwa kuongoza sheria ya kimataifa ya tabianchi siku zijazo.
5. Uchafuzi wa taka za plastiki
Mazungumzo yaliyofadhiliwa na Umoja wa Mataifa ya kukabiliana na janga la uchafuzi wa plastiki duniani yalisogea karibu na makubaliano katika mazungumzo yaliyofanyika Busan, Korea Kusini.
Mafanikio muhimu yalifanywa katika mazungumzo ya Novemba 2024 duru ya tano ya mazungumzo kufuatia azimio la Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa la 2022 linalotaka kuwepo kwa chombo cha kisheria cha kimataifa kuhusu uchafuzi wa plastiki, ikiwa ni pamoja na mazingira ya baharini.
Makubaliano yanahitajika katika maeneo matatu muhimu: bidhaa za plastiki, ikiwa ni pamoja na kemikali, uzalishaji na matumizi endelevu, na ufadhili.

Wafanyakazi wa kike wakichanganua chupa za plastiki katika kiwanda mjini Dhaka, Bangladesh.
Nchi Wanachama sasa lazima zitafute suluhu za kisiasa kwa tofauti zao kabla ya kikao kuanza tena na kufikia makubaliano ya mwisho ambayo yatashughulikia mzunguko mzima wa maisha ya plastiki na kukabiliana na kasi ya kimataifa ya kukomesha uchafuzi wa plastiki.
"Ni wazi kwamba dunia bado inataka na inadai kukomeshwa kwa uchafuzi wa plastiki," amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira UNEP, Inger
Andersen. "Tunahitaji kuhakikisha kwamba tunatengeneza chombo ambacho kinashughulikia tatizo kwa nguvu badala ya kushindwa kutimiza uwezo wake. Natoa wito kwa nchi wanachama wote kufanya sehemu yao."
No comments