Baraza la Usalama la UN lajadili ongezeko la tishio la ugaidi Afrika

Baraza la Usalama la UN lajadili ongezeko la tishio la ugaidi Afrika
Watu walio hatarini nchini Nigeria mara nyingi ni manusura na waathiriwa wa vitendo vya kigaidi.
© OCHA/Christina Powell
 
Watu walio hatarini nchini Nigeria mara nyingi ni manusura na waathiriwa wa vitendo vya kigaidi.

Afrika, kwa masikitiko makubwa, bado ni kitovu cha ugaidi wa kimataifa, na juhudi zaidi zinahitajika kutekeleza ahadi za kimataifa za kupambana na janga hili, amesema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati huu ambapo takwimu zinaonesha Burkina Faso ni ya kwanza duniani kwa idadi kubwa ya vifo vitokanavyo na ugaidi.

Baraza lilikutana leo jijini New York, Marekani kwenye kikao kilichoitishwa na Algeria, inayoshikilia Urais wa Baraza kwa mwezi huu wa Januari ili kujadili jinsi ya kuimarisha juhudi za kupambana na ugaidi barani Afrika.

Amesisitiza kuwa Baraza lina jukumu muhimu katika kuunga mkono juhudi za Muungano wa Afrika (AU) za kupambana na ugaidi, zinazoongozwa na Afrika yenyewe kwa kutumia majawabu ya kiafrika

Kuenea kwa mauaji

Bi. Mohammed amesema kwa sasa ugaidi ni tishio kubwa zaidi kwa amani, usalama, na maendeleo endelevu barani Afrika, na ametoa takwimu za kutisha zinazodhihirisha athari zake mbaya.

Licha ya juhudi zinazoendelea za nchi wanachama, nchi za Afrika zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara zinabeba takribani asilimia 59 ya vifo vyote vinavyohusiana na ugaidi duniani.

Ukanda wa Sahel ni kiini cha mgogoro mmoja mbaya zaidi duniani.  Vifo vinavyohusiana na ugaidi katika eneo hilo vimevuka 6,000 kwa miaka mitatu mfululizo, na kufanya zaidi ya nusu ya vifo vyote duniani.

Burkina Faso yaongoza duniani kwa vifo vingi vitokanavyo na ugaidi

Katika ongezeko hili, Burkina Faso sasa inaongoza duniani kwa vifo vya ugaidi, ikiwa na ongezeko la kushangaza la asilimia 68.

Wakati huo huo, vikundi vya siku nyingi vya kigaidi ambavyo ni Al-Qaeda na ISIL vimeenea katika nchi za pwani za Afrika Magharibi, huku mashambulizi ya kikatili yakiongezeka kwa zaidi ya asilimia 250 ndani ya miaka miwili.

Vitisho vya zamani na vipya

“Wakati huohuo, kundi jipya linalojulikana kama ‘Lakurawa’ linafanya mashambulizi ya kuvuka mipaka kaskazini magharibi mwa Nigeria, Niger, na Chad,” amesema Naibu Katinu Mkuu.

“Kuna pia hatari zinazoongezeka za uingizaji na msimamo mkali katika maeneo ya kaskazini mwa Ghana, pamoja na Togo, Côte d’Ivoire, na Nigeria.”
Tishio hilo linaendelea pia kwingineko, huku vikundi kama Al-Shabaab nchini Somalia, Allied Democratic Forces (ADF) katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na Ahlu Sunna Wal Jama nchini Msumbiji vikiendelea kusababisha ukatili mkubwa.

Bi. Mohammed amekumbusha kuwa vikundi hivi havijengi hofukwa jamii pekee, bali pia vinatenda ukatili wa kingono na kijinsia, pamoja na kuwashambulia watoto na kuwalazimisha kujiunga na vikundi vyao.

Kamishna wa Muungano wa Afrika, (AU) akihusika na Masuala ya Kisiasa, Amani na Usalama, Balozi Bankole Adeoye.
UN Photo/Manuel Elías
 
Kamishna wa Muungano wa Afrika, (AU) akihusika na Masuala ya Kisiasa, Amani na Usalama, Balozi Bankole Adeoye.

Afrika Magharibi hatarini

“Tusifanye makosa. Kwa kasi hii, huko Afrika Magharibi, mustakabali uko hatarini. Vijana kuenguliwa, pamoja na ukosefu mkubwa wa ajira, umewafanya kizazi kizima kuwa katika hatari ya kujiunga na vikundi vya misimamo mikali,” ameonya.
“Iwapo hatutachukua hatua, tunahatarisha kupoteza kizazi hiki kwa ugaidi, mustakabali wao ukiibwa hata kabla ya kupata nafasi ya kuanza maisha yao.” Pamoja na kutambua changamoto ya kuchukua hatua, Bi. Mohammed amesisitiza kwamba “ugaidi unavyobadilika, ndivyo nasi tunavyopaswa kubadilika.”

Ubunifu na hatua

Amesema kukabiliana vyema na ugaidi barani Afrika lazima kuhusishe ubunifu – kwa mbinu inayozingatia haki za binadamu na utawala wa sheria.

Ameelezea kuhusu Mkataba wa Zama Zijazo ulioidhinishwa Septemba mwaka jana na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, ambao unatoa msukumo mpya kwa juhudi za kimataifa dhidi ya ugaidi.
“Sasa ni wakati wa kutimiza ahadi ambazo hazijatimizwa na kutekeleza ahadi zilizotolewa katika Mkataba kwa hatua thabiti,” amesema.

Ameorodhesha maeneo matatu ya kipaumbele, akianza na kushughulikia vichocheo vya ugaidi, ambao “huimarika kwa udhaifu na kujilisha kutokana na umaskini, ukosefu wa usawa na kutoridhika.”

Pia amesisitiza umuhimu wa “mbinu za kukabiliana na ugaidi zinazozingatia haki za binadamu, zenye misingi ya uwajibikaji na taasisi shirikishi.”

Hatimaye, ametilia mkazi umuhimu wa ushirikiano wa kikanda na kuhakikisha juhudi hizi “zinaenda sambamba, zikiwa na lengo moja, na zenye mkakati ulioratibiwa.”

Ufadhili endelevu ni muhimu

Kamishna wa Muungano wa Afrika, (AU) akihusika na Masuala ya Kisiasa, Amani na Usalama, Balozi Bankole Adeoye, ni miongoni mwa wazungumzaji katika mkutano huo.

Balozi Adeoye amesema kuwa mwaka jana, Kituo cha Kupambana na Ugaidi cha AU (AUTUC) kilirekodi zaidi ya mashambulizi ya kigaidi 3,400 barani Afrika ambayo yalisababisha zaidi ya vifo 13,900.

Amesema AU “imebadilisha mkakati wake wa kimkakati wa kukabiliana na mienendo ya ugaidi” na “kuboresha” nyaraka za sera, hasa kutokana na makadirio ya ongezeko la asilimia 10 hadi 15 la ugaidi mwaka huu.

Ameongeza kuwa AU na UN zinapaswa kushirikiana ili kusaidia ufadhili unaotabirika, endelevu, na unaobadilika kwa ajili ya utekelezaji wa amani katika muktadha wa kupambana na ugaidi.

Kwa hivyo, “utekelezaji wa haraka” wa Azimio la Baraza 2719 (2023) – linalofungua mlango kwa ujumbe wa usaidizi wa amani unaoongozwa na Afrika kupata ufadhili wa UN – “utakuwa hatua kubwa mbele kwa Muungano wa Afrika katika juhudi zake za kupambana na ugaidi barani kote.”

No comments