Zahma ya Mabadiliko ya Tabianchi imewadia yaonya ripoti Mpya ya UN

Zahma ya mabadiliko ya tabianchi imewadia yaonya ripoti mpya ya UN, 24 Oktoba 2024
Mitambo ya nishati ya mafuta ni mojawapo ya watoaji wakubwa zaidi wa gesi chafu zinazosababisha mabadiliko ya hali ya hewa.
© Unsplash/Nik Shuliahin
 
Mitambo ya nishati ya mafuta ni mojawapo ya watoaji wakubwa zaidi wa gesi chafu zinazosababisha mabadiliko ya hali ya hewa.
 Tabianchi na mazingira

Uzalishaji wa hewa chafuzi wa kila mwaka uko juu sana, na hatua za haraka lazima zichukuliwe ili kuzuia ongezeko kubwa la joto na kuepuka zahma kubwa zaidi ya mabadiliko ya tabianchi, kulingana na ripoti mpya iliyotolewa leo na Shirika la Umoja wa Maataifa la Mpango wa Mazingira UNEP.

Kwa kifupi, nchi lazima zianze kuzuia utoaji wa hewa chafuzi mara moja, kulingana na Ripoti hiyo ya Pengo la Uzalishaji ya Umoja wa Mataifa 2024.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP Inger Andersen amesema "Wakati wa mabadiliko ya tabianchi umefika. Tunahitaji uhamasishaji wa kimataifa kwa kiwango cha juu na kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa hapo awali, kuanzia sasa hivi kabla ya duru inayofuata ya ahadi dhidi ya mabadiliko ya tabianchi."

La sivyo ameonya kwamba, lengo la nyuzi joto 1.5°C la kupunguza viwango vya joto vilivyowekwa katika Mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi "litakufa hivi karibuni, na la chini ya nyuzi joto mbili litakuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi".

Malengo ya tabianchi yanaweza kuyeyuka

Ilizinduliwa katika mkutano wa kimataifa wa bioanuwai wa COP16 huko Cali, Colombia, ripoti hiyo inafuatilia pengo kati ya wapi uzalishaji wa hewa chafu duniani unaelekea na ahadi za sasa za nchi na ambazo zinafaa kupunguza ongezeko la joto hadi chini ya nyuzi joto 2°C na kufuata 1.5°C sambamba na malengo ya joto yaliyowekwa katika Mkataba wa Paris wa 2015 juu ya mabadiliko ya tabianchi.

Kulingana na ripoti hiyo, lengo la nyuzi joto 1.5°C litatoweka ndani ya miaka michache ijayo endapo mataifa kwa pamoja hayatojitolea kupunguza asilimia 42 ya uzalishaji wa gesi chafu kwa mwaka ifikapo 2030 na asilimia 57 ifikapo 2035 katika awamu inayofuata ya michango iliyoamuliwa kitaifa na kuunga mkono hili na hatua za haraka.

Michango hii inaangazia hatua za kupunguza uzalishaji na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kutokana na ukame, mafuriko na matukio ya mabadiliko ya tabianchi, kupata fedha zinazohitajika na kusahihisha mipango kila baada ya miaka mitano, siku zijazo ikiwa mapema 2025 kabla ya mazungumzo ya tabianchi ya COP30 nchini Brazili.

Joto huenda likapanda hadi nyuzi 3.1°C

Bila kupunguzwa kwa kasi kwa uzalishaji wa gesi chafuzi, dunia inaweza kukabiliwa na ongezeko la joto la nyuzi joto 3.1°C lisiloepukika na la janga, kulingana na ripoti hiyo, ambayo inakuja wakati serikali zinashindwa kutekeleza kikamilifu ahadi zao.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres aesema pengo la utoaji wa hewa chafu sio dhana ya kufikirika akisistiza kwamba hakika, kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kuongezeka kwa hewa chafu na kuongezeka kwa majanga ya tabianchi ya mara kwa mara na makubwa.

"Tunateleza kwenye kamba ngumu ya dunia hii," ameonya Katibu Mkuu katika ujumbe wake wa video.

Ameongeza kuwa "Ni ama viongozi wazibe pengo la utoaji wa hewa chafu au tunatumbukia katika janga la mabadiliko ya tabianchi, huku maskini zaidi na walio hatarini zaidi wakiteseka zaidi.”

Teknolojia za gharama nafuu zinaweza kusaidia

Mkutano wa COP29 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya tabianchi unaoanza mjini Baku, Azerbaijan, mwezi Novemba unapaswa kutumika kama sehemu ya uzinduzi wa mjadala wa kina wa mipango mipya ya kitaifa kama hiyo, amesema Katibu Mkuu na kuongeza kuwa tukio hilo "linaanza sasa kwa nchi kutoa mipango mpya ya kitaifa ya tabianchi ifikapo mwakani. Serikali zimekubali kuoanisha mipango hii na nyuzi joto 1.5."

Umeme unaozalishwa na mashamba ya upepo hupunguza utegemezi wa nishati inayotumia makaa ya mawe.
© Unsplash/Fabian Wiktor
 
Umeme unaozalishwa na mashamba ya upepo hupunguza utegemezi wa nishati inayotumia makaa ya mawe.

Hiyo ina maana kwamba lazima waondoe uzalishaji wote wa gesi chafuzi na kulinda uchumi mzima, kusukuma maendeleo katika kila sekta, amesema, akizitaka nchi zenye uchumi mkubwa zaidi ambazo ni wanachama wa G20 wanaohusika na karibu asilimia 80 ya uzalishaji wote wa gesi chafuzi kuongoza katika mchakato huu.

Kuna matumaini, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisisitiza.

"Ripoti ya leo inaonyesha, teknolojia za gharama nafuu zilizopo zinaweza kufikia upunguzaji wa hewa chafu tunayohitaji ifikapo mwaka 2030 na 2035 ili kufikia kikomo cha nyuzi joto 1.5 ° C, lakini tu kwa kuongezeka kwa hamasa na usaidizi,"

Nishati safi inaweza kubadilisha mwelekeo

Ripoti hiyo inaonyesha uwezekano mkubwa wa kupunguza utoaji wa hewa chafu kwa hadi gigatoni 31 za hewa ukaa ifikapo 2030, ambayo inatafsiriwa kuwa karibu asilimia 52 ya uzalishaji ulioripotiwa mwaka 2023, na gigatoni 41 kufikia 2035, kusaidia kufikia lengo la nyuzi joto 1.5 ° C kwa miaka yote miwili.

Kwa mujibu wa ripoti kuongeza matumizi ya nishati ya jua na nishati ya upepo kunaweza kuchangia asilimia 27 ya upunguzaji wa jumla mwaka wa 2030 na asilimia 38 kufikia 2035.

Zaidi ya hayo, uhifadhi wa misitu unaweza kuchangia karibu asilimia 20 ya upunguzaji unaohitajika katika miaka yote miwili.

Mikakati mingine madhubuti ni pamoja na kuongeza ufanisi wa nishati, kuweka umeme katika sekta mbalimbali na kubadilisha kutoka kwenye matumizi ya nishati ya mafuta katika majengo, usafiri na viwanda, kulingana na ripoti hiyo.

Hata hivyo, ripoti hiyo imesema kutambua hata sehemu ndogo ya uwezo huu kutadai ushirikiano wa kimataifa ambao haujawahi kushuhudiwa na mbinu kamili kutoka kwa serikali, zikilenga katika kuongeza manufaa ya kijamii, kiuchumi na kimazingira huku kukiwa na kupunguza mgawanyiko wa kibiashara.

No comments