Umoja wa Mataifa wasema kinachotokea Ukingo wa Magharibi na Jerusalemu Mashariki dhidi ya Wapalestina ni ubaguzi wa rangi
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu OHCHR imetoa ripoti ya kina hii leo jijini Geneva Uswisi ikieleza hali ya haki za binadamu katika eneo la Ukingo wa Magharibi pamoja na Jerusalemu Mashariki huko Mashariki ya Kati eneo linalokaliwa kwa mabavu na Israel ambapo kumerekodiwa athari za ukandamizwaji wa sheria, sera na mienendo ambao unawaathiri katika kila nyanja ya maisha ya kila siku ya Wapalestina waishio maeneo hayo.
Ripoti hiyo, inaonya kuwa Israel inakiuka sheria za kimataifa zinazotaka mataifa kupiga marufuku na kutokomeza aina zote za ubaguzi wa rangi kwa namna ambavyo utekelezaji wa sera hizo umeimarishwa na kuathiri maisha ya wapalestina.
Ripoti inaeleza kuwa ubaguzi wa kimfumo dhidi ya wapalestina ni wa muda mrefu na kwamba hali imezorota sana tangu mwezi Desemba 2022, huku maisha ya Wapalestina yakizidi kubanwa na kutokuwa salama.
Ripoti inasema walowezi wa Israel na wapalestina wanatawaliwa na mifumo tofauti ya sheria na sera, hali inayosababisha ukosefu wa usawa katika harakati na upatikanaji wa rasilimali, huku wapalestina wakinyang’anywa ardhi, makazi na kunyimwa haki za msingi kupitia mahakama za kijeshi.
Ripoti pia inasema kuwa utengaji na ubaguzi dhidi ya wapalestina unaonekana kukusudiwa kuwa wa kudumu, jambo linalokiuka Kifungu cha 3 cha mkataba wa kimataifa wa kuondoa aina zote ya ubaguzi wa rangi (ICERD) kinachokataza ubaguzi wa rangi na apartheid.
Ripoti inaeleza kuwa tangu tarehe 7 Oktoba 2023, kumekuwepo na ongezeko kubwa la matumizi ya nguvu haramu, kukamatwa kiholela, vizuizi vya harakati, upanuzi wa makazi na vurugu za walowezi, hali iliyosababisha kuzorota kwa kiwango kikubwa cha haki za binadamu katika ukingo wa magharibi unaokaliwa.
Aidha, ripoti inaandika mienendo ya mauaji haramu na aina nyingine za vurugu za dola na walowezi, ikijumuisha mifano mingi ya matumizi ya nguvu ya kuua yaliyotumika bila sababu, kwa njia ya kibaguzi dhidi ya wapalestina, na kwa nia dhahiri ya kuua.
Vizuizi vya kibaguzi vinazuia wapalestina kufikia ardhi zao, kuathiri kipato chao, huku ujenzi wa barabara za walowezi na kufukuzwa makazi ukiwa ni uhamisho haramu unaoathiri jamii zao.
Ripoti inasema wapalestina wananyimwa rasilimali zao, hasa maji, kupitia unyang’anyi na ubomoaji wa miundombinu, hali inayowalazimisha kununua maji kutoka kampuni ya serikali ya Israel.
“Kuna kukabwa kwa utaratibu kwa haki za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi, akiongeza kuwa kila nyanja ya maisha kupata maji, elimu, huduma za afya, kutembelea familia au kuvuna mizeituni inadhibitiwa na kubanwa na sera za kibaguzi.” amesema Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN, Volker Türk
Ripoti pia inaonesha kuwa kutokuwajibishwa kunatawala kwa ukiukwaji wa haki za binadamu. Kati ya mauaji zaidi ya 1,500 ya wapalestina kati ya Januari 2017 na Septemba 2025, mamlaka za Israel zilifungua uchunguzi 112 pekee, huku hukumu moja tu ikitolewa. Maelfu ya wapalestina bado wanashikiliwa kiholela, wengi chini ya “kizuizi cha kiutawala,”bila mashtaka wala kesi.
Upanuzi haramu wa makazi ya walowezi unaendelea bila kukoma, huku makumi ya maelfu ya hekta za ardhi ya wapalestina zikinyakuliwa kwa ajili ya makazi mapya. Türk ametoa wito kwa Israel kubatilisha sheria, sera na mienendo yote inayodumisha ubaguzi wa kimfumo, kukomesha uwepo wake haramu katika ardhi ya Palestina inayokaliwa, kuvunja makazi yote, kuwaondoa walowezi, na kuheshimu haki ya watu wa Palestina ya kujitawala.
Chanzo UN
No comments