*TUMIENI MAPATO YA NDANI KUBORESHA MINADA NA MABWAWA- RC MAKALLA*
*_Asema Longido ni Wilaya ya Wafugaji, Kuboresha minada na mabwawa kutachochea Biashara na ufugaji._*
*_Aagiza kupelekwa mtambo wa kuchimba visima na mabwawa kufuatia changamoto ya ukame_*
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla ameuagiza Uongozi na Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Longido kutoa kipaumbele kwenye sekta ya Ufugaji kwa kuwekeza kwenye ujenzi wa miundombinu ya mabwawa, majosho na minada ili kutoa huduma bora kwa wananchi na kuongeza mapato ya Halmashauri hiyo.
Mhe. Makalla ametoa kauli hiyo leo Jumanne Disemba 23, 2025 alipokutana na Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Longido, ambapo pamoja na mambo mengine alielezwa kuhusu changamoto ya ukame na namna inavyowaathiri wafugaji wa Wilaya ya Longido pamoja na kukauka kwa mabwawa kutokana na yaliyokuwepo kujaa matope.
"Ni maelekezo yangu kwamba Mkurugenzi na Madiwani tengeni fedha yaangalieni mabwawa haya. Uchumi na mapato yenu yanategemea mifugo nendeni mkawekeze huko na ni maelekezo yangu kwa Halmashauri muelewe kuwa mna Wilaya ya Wafugaji, minada isimamiwe na kuboreshwa na uhakika wa maji kwa wafugaji uwepo kupitia mapato yenu ya ndani." Amesema Mhe. Makalla.
Katika hatua nyingine Mhe. Makalla amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Ndg. Musa Albano Missaile kusimamia kwa haraka upelekaji wa Mitambo ya uchimbaji wa visima Wilayani humo ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji katika Wilaya hiyo kutokana na msimu wa mvua kuchelewa katika maeneo hayo.
Mapema katika kikao hicho maalumu cha Baraza la Madiwani, Mbunge wa Jimbo la Longido, Dkt. Steven Kiruswa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Ndg. Thomas Ngobei wamemueleza Mhe. Makalla kuhusu ukame uliopo Wilayani humo, wakimuomba kuwasaidia wafugaji wa Wilaya hiyo kuweza kupata huduma ya maji kwaajili ya mifugo yao.
No comments