WAZIRI TAMISEMI AAGIZA MIRADI YA TACTIC ARUSHA KUKAMILIKA KWA WAKATI
Amshukuru Rais Samia kwa uwekezaji wake Mkoani Arusha
Ataka uwazi ugawaji wa Vizimba soko likikamilika
Rc Makalla aahidi kusimamia miradi hiyo kukamilika kwa wakati
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe ameuagiza Uongozi wa Jiji la Arusha kuhakikisha wafanyabiashara waliokuwepo kwenye Soko la Kilombero wanapewa kipaumbele pindi soko hilo litakapokamilika, akitaka uwazi pia wakati wa ugawaji wa vizimba katika soko hilo.
Mhe. Prof. Shemdoe amebainisha hayo leo Alhamisi Disemba 18, 2025 wakati wa ziara yake ya siku mbili Mkoani Arusha, mradi unaotekelezwa kupitia Mradi wa uendelezaji Miji Tanzania (TACTIC) unaohusisha ujenzi wa soko hilo, ujenzi wa soko la Morombo na Kituo Kikuu cha mabasi kinachojengwa Bondeni City Jijini hapa.
"Hapa Arusha kwa miradi inayoendelea hapa ya Bilioni 30 ikihusisha masoko na stendi inaonesha namna ambavyo Rais wetu Dkt. Samia anavyotujali wana Arusha, kwahiyo tumshukuru sana na tuendelee kumshukuru Jemedari wetu Mkuu wa Mkoa kwa usimamizi wake mkubwa anaoufanya na hakika kazi inaendelea na ninyi wana Arusha ni mashahidi wa kazi kuendelea."
"Nitoe maelekezo kwa Viongozi wa Jiji soko hili litakapofunguliwa tuhakikishe kwamba wale waliokuwa hapa mwanzo ndio wanapewa kipaumbele kwenye ugawaji wa vizimba na hili nitalifuatilia na kama kuna Afisa biashara atakwenda kinyume na hili kazi yake nitaondoka nayo.Niagize pia uwazi kwenye Vizimba vitakavyobaki nakemea tabia ya baadhi ya Viongozi kubeba vizimba na kukodisha kwa wananchi ili kupata cha ziada." Amesema Prof. Shemdoe.
Kwa upande wake Mhe. Makalla ameeleza utayari wake wa kusimamia maelekezo ya Waziri Shemdoe, akisema matarajio ya wananchi kwa serikali ni makubwa na jukumu lake muhimu ni kuhakikisha mradi huo unakamilika kufikia Mei 2026 kama ilivyo kwenye Mkataba ili kutimiza matarajio ya wananchi wa Mkoa wa Arusha.*
No comments