ARUSHA KULIKUWA NA VURUGU NA UPORAJI SI MAANDAMANO- RC MAKALLA
Aeleza maana ya maandamano
Aalika taasisi na watalii kufanya mikutano na kutalii mkoani Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla amesema kilichofanyika Mkoani Arusha na katika baadhi ya Miji na Majiji ya Tanzania Oktoba 29, 2025 ni vurugu, uporaji na uharibifu na si maandamano.
Mhe. Makalla ameyasema hayo leo Novemba 30, 2025 mbele ya Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwenye mkutano wa hadhara kwenye Viwanja vya Magufuli, Arumeru, akieleza kuwa katika vurugu hizo, maduka yalivunjwa, bidhaa kuibiwa, uporaji wa fedha pamoja na uchomaji wa Vituo vya kuuza mafuta, magari, Majengo ya Polisi na mahakama za ngazi mbalimbali katika Mkoa wa Arusha na maeneo mengine.
Akinukuu kamusi ya Kilatini, Mhe. Makalla amesema Maandamano ni kikundi cha watu wanaotembea pamoja kwa utaratibu maalum na ujumbe maalum, akisema kuwa kamwe Mkoa wa Arusha hautaruhusu vurugu kujitokezs tena na akiwakaribisha Watalii na Taasisi mbalimbali kufika Mkoani Arusha ili kutalii pamoja na kufanya mikutano yao na kuwahakikishia amani na usalama wa kutosha.
Awali Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amekagua Kituo cha Polisi, Mahakama, Vituo vya kuuza mafuta pamoja na maeneo mengine yaliyochomwa moto wakati wa vurugu hizo za Oktoba 29, 2025 na kuzungumza na wananchi, akiwahimiza kulinda amani iliyopo nchini na kutokubali kurubuniwa na wachache wenye kuhatarisha amani ya Tanzania kutokana na maslahi yao binafsi.
No comments