TAMWA YAWAPONGEZA WANAWAKE WALIOJITOKEZA KUWANIA UONGOZI UCHAGUZI MKUU
Dar es Salaam
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimewapongeza wanawake
wote waliojitokeza kuwania nafasi za uongozi kuanzia udiwani, ubunge
hadi urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Kwa
mujibu wa takwimu za Ulingo Wanawake, jumla ya wanawake 231 walichukua
fomu za ubunge kupitia CCM, ambapo 25 kati yao wameteuliwa kugombea,
nane wakiwa ni wapya. Aidha, vyama mbalimbali vya siasa mwaka huu
vimeongeza idadi ya wanawake walioteuliwa kuwa wagombea wenza katika
nafasi ya urais na makamu wa rais.
Kwa
mara ya kwanza katika historia ya chama tawala, CCM imemteua Mheshimiwa
Samia Suluhu Hassan kugombea urais, hatua ambayo TAMWA imeielezea kuwa
ya kihistoria na inayoashiria mwelekeo mpya wa ushiriki wa wanawake
katika uongozi wa juu nchini.
Mbali
na Samia, wanawake wengine walioteuliwa kugombea nafasi ya urais ni
pamoja na Mwajuma Noty Mirambo wa UMD aliyekuwa na mgombea mwenza
Mashavu Alawi Haji. Wagombea wenza wanawake kutoka vyama vingine ni
pamoja na Eveline Wilbard Munis (NCCR-Mageuzi), Husna Mohamed Abdallah
(CUF), Aziza Haji Selemani (MAKINI), Amani Selemani Mzee (TLP), Chausiku
Khatibu Mohamed (NLD), Sakia Mussa Debwa (SAU), Chuma Juma Abdallah na
Devotha Minja (CHAUMA).
Akizungumza
kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA,
Dkt. Rose Reuben, alisema chama hicho kinatambua ujasiri wa wanawake
waliothubutu kugombea licha ya changamoto mbalimbali wanazokabiliana
nazo, ikiwemo mfumo dume na udhalilishaji, hasa kwenye mitandao ya
kijamii.
Taarifa
za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha hadi Februari 2024,
wanawake walikuwa asilimia 37.4 ya wabunge (148 kati ya 392), wengi
wakiwa kupitia viti maalum. Ripoti za Aprili na Julai 2024 pia
zinaonyesha kuwa wanawake walikuwa asilimia 37.5 ya mawaziri nchini.
TAMWA
imeeleza kuwa licha ya mafanikio haya, bado kuna changamoto kubwa
katika kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu kwenye siasa na
uongozi. Chama hicho kimeendelea kutoa elimu kupitia warsha, makongamano
na vyombo vya habari ili kuhakikisha wanawake wanashiriki katika
mazingira yenye usawa na usalama.
“Uwepo
wa wanawake katika uongozi ni muhimu kwa maendeleo ya taifa kwani
huongeza uwajibikaji, usawa wa kijinsia na kulinda maslahi ya makundi
yote hususan wanawake na watoto,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha,
TAMWA imetoa wito wa kampeni safi, zenye staha na jumuishi, ikisisitiza
kuwa itafuatilia mwenendo wa kampeni na kuripoti ukiukwaji wowote wa
kanuni za uchaguzi ili hatua za kisheria zichukuliwe.



No comments