Kuvunja mifumo kandamizi dhidi ya wanawake ni mapinduzi ya aina yake – Balozi Mongella
Ikiwa ni miaka 30 tangu kufanyika kwa mkutano wa 4 wa kimataifa kuhusu masuala ya wanawake huko Beijing, China, Balozi Gertrude Mongella, ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa mkutano huo amesema elimu inasalia bado msingi wa kumkomboa mwanamke dhidi ya mifumo kandamizi iliyojikita katika maeneo mbalimbali.
“Wanawake tusibaki nyuma kwenye elimu ya kawaida,” amesema Balozi Mongella akisema “hii itatukosesha mambo mengi. Serikali zetu ziangalie jinsi ya kujumuisha wanawake kwenye sayansi ya TEHAMA na dijitali.”
Nilipoteuliwa sikuona sababu ya kulalamika na kulialia
Alipoulizwa tafakuri aliyokuwa nayo baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa mkutano huo, Balozi Mongella amesema, “nilitafakari na kuona kuwa nimepewa jukumu la dunia nzima, kwa hiyo masuala ya kulalamika lalamika na kulialia nikaona havitanikifisha popote ni bora kuanza kuweka mikakati.”
Anasema aliunda kamati mbali mbali zilizokutana na kujadili na kisha kuwa na ajenda mahsusi ambazo zinagusa wanawake wote, “kwa sababu maslahi ya wanawake ni ya muhimu katika jamii nzima.”
Maeneo waliyogusa ni pamoja na elimu, afya na ushiriki wa wanawake katika maamuzi kuanzia ngazi ya familia mpaka ngazi za uongozi wa kisiasa. Halikadhalika upatikanaji wa rasilimali kwa wanawake ili waweze kujiendesha waweze kujiimarisha kiuchumi bila ya kutoa umasikini miongoni mwa wanawake.
Balozi Mongella amesema hilo ni muhimu, “Kwa sababu hata katika mataifa yaliyoendelea bado unakuta wanawake ndio maskini wa masikini. Halikadhalika unyanyasaji wa kijinsia tuliuweka kama ni suala muhimu la kuangalia sasa wanawake popote duniani wananyanyaswa. Kama wewe unapigwa unaita polisi na angalau mwenzio akipigwa anapiga yowe. Wote huo ni unyanyasaji.”
Harakati za wanawake na vijana wa kike
Balozi Mongella ambaye naye ametimiza umri wa miaka 80 kama Umoja wa Mataifa, aliulizwa mtazamo wake wa harakati za wanawake na wasichana wa zama za sasa katika utetezi wa haki ambapo amesema zina mwelekeo sawa lakini ni vema kupunguza mhemuko.
“Kinachonisikitisha ni kuwa vijana wa sasa wana mihemko, wanafanya mambo kwa mihemko na ile hali haidumu. Tukitaka mabadiliko ya kweli huwezi kuwa na mhemko unaenda kwa misingi, na iwe misingi itakaweza kutufanya tujitegemee,” amesema Balozi Mongella.
Kubadili mifumo ni mapinduzi ya aina yake, tusikate tamaa
Kuhusu changamoto za kufikia azimio la Beijing kwa asilimia 100, Balozi Mongella ametaja changamoto kuwa ni pamoja na kwamba, “huu ubaguzi wa wanawake umejengeka ndani ya mifumo ya siasa umejengeka ndani ya mifumo ya uchumi, imani na mifumo yote inayotawala maisha ya binadamu.”
Ametambua kuwa “ni kazi kubwa kubadilisha mifumo yote ambayo imekuwepo kwa muda mrefu. Ni vigumu kuibadilisha yote kwa siku moja. Ndiyo maana lazima tuvute subira kama tunataka kwenda kwa njia ambayo ni sahihi. Na hayo ni lazima tutambue ni mapinduzi ya aina yake.”
Ametanabaisha kuwa harakati zinatofautiana, “kuna wakati utaenda kasi na kuna wakati inabidi uende taratibu na kwa uangalifu zaidi katika kuweka mifumo mipya na mimi ninafikiri ya kwamba tutaweza na tusikate tamaa.”
Balozi Mongella ametumia mahojiano kushukuru Mungu kwa vipaji alivyompatia hadi kuweza kufanikisha mkutano huo wa kihistoria
No comments