UTEUZI WA MWISHO WAGOMBEA UBUNGE, UDIWANI CCM KUFANYIKA JULAI 28
UTEUZI WA MWISHO WAGOMBEA UBUNGE, UDIWANI CCM KUFANYIKA JULAI 28

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla
Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kuwa kikao cha mwisho cha uteuzi wa
wagombea wake wa nafasi za Ubunge na Udiwani kimepangwa kufanyika tarehe
28 Julai, 2025, badala ya Julai 19 kama ilivyokuwa imepangwa awali.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo katika Makao Makuu ya chama hicho jijini
Dodoma, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla,
amesema mchakato wa maandalizi ya uchaguzi ndani ya chama hicho
unaendelea kwa mafanikio huku ukihitaji umakini mkubwa kutokana na wingi
wa wagombea.
“Leo
wengi walitarajia Kamati Kuu ingeketi kwa ajili ya uteuzi, lakini sasa
shughuli hiyo imepangwa kufanyika Julai 28. Hili ni zoezi nyeti
linalohitaji umakini mkubwa, na ndiyo maana tumeamua kujipa muda zaidi
ili tuweze kufanya kazi hii kwa weledi,” amesema Makalla.
Kwa
mujibu wa Makalla, vikao muhimu vya maamuzi vitafanyika kuanzia Julai
26 hadi Julai 28, 2025, ambapo Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM (CC)
itakutana Julai 26, ikitanguliwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa
(NEC), ambacho kitaweka bayana maamuzi ya awali kuhusu uteuzi.
Amesema idadi kubwa ya waliojitokeza kuwania nafasi hizo imepelekea chama kujipa muda zaidi kufanya uchambuzi wa kina.
“Kwa
mfano, wagombea wa nafasi ya udiwani ni zaidi ya 27,000, na wale wa
ubunge ni zaidi ya 10,000. Kazi ya kuchambua ni kubwa. Tunataka tutende
haki, tufanye kwa umakini na kwa utulivu,” amesema.
Ameongeza
kuwa bado hakuna mgombea yeyote aliyekatwa na kwamba kikao cha Julai 28
kitafanya maamuzi rasmi ya nani atasonga mbele kwenye hatua inayofuata
ya mchakato wa ndani wa CCM.
“Napigiwa
simu nyingi kuhusu lini uteuzi utafanyika. Nataka niwaambie, kazi
inaendelea kwa hatua makini. Hakuna aliyekatwa bado. Kikao cha Julai 28
kitaamua rasmi nani anasonga mbele,” amesema Makalla.
Aidha,
amesema baada ya uteuzi huo, chama kitapanga na kutangaza ratiba ya
kura za maoni, hatua muhimu inayofuata katika kuwapata wagombea wa
mwisho watakaowania kwa tiketi ya CCM katika uchaguzi mkuu ujao.
Makalla
amewahimiza wagombea wote waliowasilisha nia zao kuwa na uvumilivu na
utulivu, akisisitiza kuwa chama kimejipanga kutoa wagombea bora, wa
kuaminika na wenye sifa za kuwatumikia wananchi kwa uadilifu.
“Wagombea watulie, wa relax wakati tunaendelea na mchakato mpaka tarehe 28,” amesisitiza.
Uteuzi
huu ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, ambapo CCM
kama chama tawala kimesema kitaibua wagombea wake bora kwa ajili ya
kupeperusha bendera ya chama hicho katika ngazi mbalimbali kuanzia
serikali za mitaa hadi ngazi ya kitaifa
Credit Na Kadama Malunde na Dotto Kwilasa– Malunde 1 Blog
No comments