DKT. TULIA AFUNGUA KIKAO CHA JUKWAA LA KIBUNGE UN
DKT. TULIA AFUNGUA KIKAO CHA JUKWAA LA KIBUNGE UN
Spika
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge
Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, 22 Julai 2025, amefungua rasmi
Kikao cha Jukwaa la Kibunge katika Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Umoja wa
Mataifa wa Mwaka 2025 kuhusu Maendeleo Endelevu _(Parliamentary Forum at
the 2025 UN High Level Political Forum on Sustainable Development)_,
kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Umoja wa
Mataifa, New York, Marekani.
Katika
hotuba yake ya ufunguzi, Mhe. Dkt. Tulia ameeleza umuhimu wa Mabunge
duniani kushirikiana kwa karibu na Serikali zao katika kujenga mifumo
imara ya usawa wa kijinsia na afya kwa wote, sambamba na utekelezaji wa
Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususani Lengo namba 3 (Afya kwa
Wote) na Lengo namba 5 (Usawa wa Kijinsia).
Akigusia
Lengo la 3, Dkt. Tulia ameeleza kuwa bado kuna pengo kubwa katika
upatikanaji wa huduma bora za afya, hasa katika nchi zinazoendelea,
licha ya kwamba malengo haya yanatarajiwa kufikiwa ifikapo mwaka 2030.
Amehimiza haja ya ushirikiano madhubuti baina ya Serikali na Mabunge
katika kuhakikisha kwamba huduma hizo zinaboreshwa na kufikika kwa wote.
Kuhusu
Lengo la 5, Dkt. Tulia amesema licha ya mafanikio yanayoendelea
kupatikana katika kupambana na ukatili, ubaguzi na ukosefu wa ushiriki
wa wanawake katika siasa na uongozi, bado ipo kazi kubwa ya kufanya.
Amesisitiza kuwa Mabunge yana wajibu wa kuendelea kutunga na kusimamia
sheria zinazoimarisha haki, usawa, uwajibikaji na ufadhili wa kweli kwa
mipango ya kuwawezesha wanawake na wasichana ili kufikia maendeleo
jumuishi na endelevu.




No comments