VIONGOZI WA KIMAASAI WAMSIMIKA RC MAKONDA CHEO KUWA LAIGWANANI - ARUSHA

VIONGOZI WA KIMAASAI  WAMSIMIKA RC MAKONDA CHEO KUWA LAIGWANANI - ARUSHA 

Viongozi wa Mila Longido Wamtunuku Mhe. Paul Makonda Cheo cha Laigwanani wa Kimaasai
Longido, Arusha — Katika tukio la kihistoria na la kipekee, viongozi wa mila wa jamii ya Kimaasai Wilaya ya Longido leo wamemsimika rasmi Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa Paul Christian Makonda, kuwa Laigwanani wa Mila za Kimaasai. Hafla hiyo imefanyika wakati Mhe. Makonda alipokuwa akitembelea eneo la Sinya kushuhudia utiaji saini wa mkataba wa uchimbaji wa visima vya maji, kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA).

Akizungumza katika tukio hilo, Mhe. Makonda alieleza kuwa heshima hiyo aliyotunukiwa ni ya kipekee na inampa moyo wa kuendelea kushirikiana kwa karibu na jamii ya Kimaasai katika shughuli za maendeleo.

Kwa upande wao, viongozi wa kimila walieleza kuwa wametambua juhudi za Mkuu huyo wa Mkoa katika kusukuma mbele maendeleo ya wananchi, hasa katika sekta ya maji safi na usafi wa mazingira.

Katika hatua ya kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji, AUWSA imefanya utafiti wa kitaalamu na kubaini kuwa eneo bora kwa uchimbaji wa kisima kirefu ni katika kijiji cha Ildonyo, kata ya Sinya. Visima hivyo ni sehemu ya mradi mkubwa wa kuboresha huduma ya maji safi na usafi wa mazingira kwa Jiji la Arusha na maeneo ya jirani.

Mradi huu unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa maji kwa maelfu ya wakazi wa Mkoa wa Arusha, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikumbwa na uhaba wa huduma hiyo muhimu.

"Nimepokea heshima hii kwa unyenyekevu mkubwa. Hili ni deni kwangu kuhakikisha kuwa jamii hii inapata maendeleo ya kweli, hasa katika sekta ya maji, afya na elimu," alisema Mhe. Makonda.

AUWSA inaendelea kushirikiana na viongozi wa jamii na wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa huduma za msingi zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

No comments