Makamu Mwenyekiti CHADEMA Heche naye akamatwa na POLISI

Makamu Mwenyekiti CHADEMA Heche naye akamatwa na POLISI

.

Chanzo cha picha,MWZ

Makamu Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, John Heche, amekamatwa leo na Jeshi la Polisi katika eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka CHADEMA, Heche alikuwa amekwenda kuongoza mkutano wa hadhara ambao tayari ulitangazwa na taarifa yake kuwasilishwa kwa Polisi siku kadhaa zilizopita.

Hata hivyo, Polisi walileta barua saa chache kabla ya mkutano kuanza, wakipinga kufanyika kwake kwa madai kuwa eneo la mkutano Mtaa wa Nyamwezi na Mkunguni lina shughuli nyingi za biashara na mkutano huo ungeathiri shughuli hizo.

"tunashauri mkutano wenu huo wa hadhara ufanyike katika eneo lingine la wazi", ilisema barua ya Polisi kwenda CHADEMA.

Licha ya zuio hilo, Heche alifika eneo la mkutano, ambapo Polisi walimkamata na kuondoka naye. Taarifa zaidi kuhusu mahali alipo bado zinafuatiliwa na chama hicho.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Godbless Lema, amethibitisha kukamatwa kwa Heche kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani Twitter), ingawa Jeshi la Polisi halijatoa taarifa rasmi hadi sasa.

"Taarifa ya Mkutano ilipekekwa Wiki Moja Iliyopita na Mkutano ulianza kutangazwa. Leo Mchana Polisi wameleta barua kuzuia mkutano kufanyika Kariakoo", aliandika Lema.

Kukamatwa kwa Heche kunakuja wiki chache baada ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za uhaini mashtaka ambayo hayana dhamana.

Lissu anatarajiwa kufikishwa tena Mahakama ya Kisutu tarehe 24 Aprili, 2025, ambapo Heche amekuwa akihamasisha wafuasi wa CHADEMA kujitokeza kwa wingi.

Matukio haya yamezua hofu na mijadala mikali kutoka kwa wananchi na viongozi wa dini, wakitaka kuwepo kwa maridhiano ya kitaifa na utulivu wa kisiasa.

Katika kipindi hiki, CHADEMA inaendelea na kampeni yake ya “No Reform, No Election”, ikisisitiza kuwa hakutakuwa na ushiriki katika uchaguzi wowote bila kufanyika kwa mabadiliko makubwa ya kisiasa na kisheria

No comments