TAARIFA KWA UMMA KUTOKA TAASISI YA UTAFITI WA MISITU TANZANIA (TAFORI)
IMANI POTUFU JUU YA MITI AINA YA TEMINALIA (PANGA UZAZI)
UTANGULIZI
Kumekuwepo na taarifa zinazozungushwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kuhusu miti aina ya Teminalia (maarufu kama Mkungu na Panga uzazi) ikihusishwa na kusababisha majanga, chuki, ugomvi na vifo kwa jinsia ya kiume popote pale miti hii ilipopandwa au kumea. Hivyo Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) ambayo imepewa mamlaka na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kufanya, kusimamia na kuratibu tafiti za Misitu nchini kwa mujibu wa Sheria ya Bunge Namba 5 ya mwaka 1980 inapenda kutoa taarifa kwa Umma kuhusu miti aina ya Teminalia. Taarifa hii kwa umma inakuja baada ya watafiti kusikia na kuona watu wengi wakichukua maamuzi ya kuingoa miti ya Teminalia katika makazi na maeneo kutokana na kuenea kwa taarifa hizi zenye kupotosha. Tunapenda jamii ifahamu mambo yafuatayo ya msingi kuhusu miti aina ya Teminalia.
(i) Kuna aina zaidi ya 100 za miti aina ya Teminalia hapa duaniani na yote haina madhara yanayotajwa katika taarifa ambazo sio rasmi zinazozunguka katika mitandao ya kijamii.
(ii) Hata hivyo mti unaolaumiwa na kuhusishwa na imani potofu umetajwa kwa jina la kisayansi kama Terminalia catappa (Mkungu) japo picha zinazozungushwa kwenye mitandao ya kijamii ni picha za mti unaoitwa kwa jina la kisayansi kama Terminalia mantaly (Panga uzazi).
(iii) Miti ya Terminalia catappa (Mkungu) inapatikana kwa asili katika sehemu zenye joto la kiasi katika pwani za Bara la Asia. Hata hivyo imepandwa maeneo mengi katika bara la Afrika hasa karibu na maeneo ya Pwani yenye mwinuko usiozidi meta 600 juu ya usawa wa bahari, na miti aina ya Terminalia mantaly (Panga Uzazi) imepandwa kuanzia uwanda wa chini kiasi hadi maeneo yenye miinuko na baridi kama yale yanayozunguka milima ya Tao la Mashariki mwa Tanzania.
(iv) Aina hizi mbili za miti ya Terminalia zinatofauti kubwa, Terminalia catappa (Mkungu) ikiwa na majani mapana, wakati ambapo Terminalia mantaly(Panga Uzazi) majani yake ni madogo. Na pia Terminalia catappa (Mkungu) inazaa matunda makubwa yanayoliwa na wanadamu na sehemu nyingi za Tanzania mti huu umejulikana kama Mkungu, maana unazaa kungu na haujawahi kujulikana kama mti chonganishi sehemu yoyote duniani. Kwani sehemu za Asia ambapo mti huu unapatikana kwa asili unajulikana kama India almond au Sea almond, yaani Mkungu wa India au Mkungu wa sehemu za bahari.
(v) Jina la mti huu (Terminalia catappa) halina uhusiano na sehemu za siri za mwanaume. Kwani sehemu ya kwanza ya jina hili yaani Terminalia inatokana na neno la Kilatini Terminus linaloleta neno la Kiingereza Terminal, yaani ya mwishoni, cha mwishoni, mwishoni. Hii ikimaanisha kwamba majani yake yamekusanyika mwishoni kabisa mwa tawi au kijitawi. Na sehemu ya pili ya jina yaani catappa inatokana na neno Ketapang kwa lugha ya Maleshia (Malay) likimaanisha mti wenye mbegu zinazotumika kutengezea dawa. Na sehemu nyingi za Asia, ikiwemo mitaa, viwanja vya ndege, watu, wamepewa jina hili la Ketapang likiwa na maana nzuri tu kwa lugha ya Kimaleshia.
(vi) Ifahamike kwamba miti ya Terminalia catappa (Mkungu) inafaa kwa matumizi mbali mbali; magome yake na majani hutumika kuweka rangi nyeusi kwenye ngozi, mbao yake ni nzuri na hutumika kwa kutengenezea boti na ujenzi wa nyumba, mbegu zake huliwa na zinatoa mafuta yasiyo na harufu ambayo hutumika kutibu uvimbe tumboni na yakichemshwa na majani yake hutibu magonjwa mengi ya ngozi, tunda lake huliwa tena lina harufu nzuri japo kwa sababu ya nyuzi nyuzi nyingi halipendelewi sana na watu wengi, hupandwa zaidi sana kama mti wa kupendezesha mandhari kwenye miji na bustani kwani una matawi yanayosambaa kwa mlalo na majani yake ni mapana, hivyo hutoa kivuli kizuri. Mizizi ya mti huu husambaa kwa mlalo ili kuweza kushikilia mti usianguke, hivyo kama ilivyo kwa miti mingine mingi si vyema kuipanda karibu sana na nyumba kwa hofu ya kuleta nyufa kwenye majengo dhaifu.
HITIMISHO
Taasisi ya Utafiti Misitu Tanzania ingependa kuwatoa hofu wananchi juu ya miti aina ya Terminalia na kusisitiza kwamba miti hii ising’olewe kwa kisingizio cha imani potofu kwani haina madhara yanayoelezwa na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii. Miti aina zote mbili (yaani Terminalia catappa na Terminalia mantaly) inafaa kwa ajili ya bustani na kuboresha mandhari. Pia TAFORI inawasihi viongozi wa kijamii na kidini kuacha hulka ya kutafuta umaarufu kwa kutoa taarifa zisizo rasmi na zenye kupotosha jamii zinazohusisha viumbe na majanga ikiwemo miti. Wananchi wanasisitizwa wafanye kazi ili kuboresha hali ya maisha yao na mazingira lakini sio kusingizia viumbe asili kama chanzo cha majanga na matatizo yao ya kiuchumi na kijamii.
Kwa maelezo zaidi tafadhali wasiliana na:
Kaimu Mkurugenzi Mkuu,
Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania,
S.L.P. 1854,
MOROGORO - TANZANIA
Simu: +255 23 2604499
Nukushi: +255 23 2603725
Barua elekloniki: tafori@tafori.or.tz
Tovuti : www.tafori.or.tz
No comments