RAIS SAMIA ATOA DAWA ZA MILIONI 100 KAMBI YA MATIBABU YA RC MAKONDA.*

*RAIS SAMIA ATOA DAWA ZA MILIONI 100 KAMBI YA MATIBABU YA RC MAKONDA.* 

 _Madaktari 100 waongezwa, wengine zaidi ya 20 watoka Marekani_ 

 _Utaratibu maalum wa kuhudumia wazee, walemavu, watoto na wajawazito kuanza kesho_ 

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amepokea dawa za aina mbalimbali zenye thamani ya Milioni 100 zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuunga mkono Kambi maalum ya matibabu ya kibingwa inayoendelea kwenye viwanja vya Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha.

Dawa hizo zimetolewa na kukabidhiwa Mkoani Arusha, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa Mchana wa Jumatatu ya Juni 24, 2024 wakati alipopiga simu na kuzungumza na maelfu ya wananchi waliojitokeza wakati wa ufunguzi wa Kambi hiyo ya matibabu.

Katika ahadi hiyo Mhe. Rais Dkt. Samia pia aliahidi kutoa msaada wa matibabu kwa watakaoonekana kuhitaji matibabu ya ziada, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Makonda amesema kufikia leo jumla ya watu 30 tayari wamepata rufaa ya kupelekwa kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na Hospitali nyingine za Kanda.

"Tumshukuru Mhe. Rais kwa kujitoa kwake, lakini  jambo jingine pia tusiache kumuomba Mungu. Madaktari wana nafasi zao, serikali ina nafasi yake na Mungu ana nafasi yake. Tusiache kumuomba Mungu atusaidie ili hizi dawa tunazopewa ziweze kuleta tija katika afya zetu." ameongeza Mhe.Makonda.

Katika Hatua nyingine Mhe. Paul Christian Makonda leo Juni 26, 2024 ametangaza kuongeza madaktari wengine 100 kando ya wahudumu wa afya na madaktari 450 waliokuepo awali, akisema lengo ni kuongeza kasi na ufanisi katika kuwahudumia wananchi wenye uhitaji wa vipimo pamoja na matibabu.

Aidha Mhe. Paul Christian Makonda pia ametangaza kuongeza vitenganishi vya maabara pamoja na mahema ya kuhudumia wananchi kutokana wingi Mkubwa wa watu wanaojitokeza kila uchao kwaajili ya kuhudumiwa kwenye kambi hiyo.

Mhe. Makonda pia ametangaza uwepo wa wahudumu wa afya na madaktari wanafunzi takribani 25 kutoka nchini Marekani ambao wamefika Mkoani Arusha, kwenye kambi hiyo ya Matibabu inayotarajiwa kufikia tamati mwishoni mwa juma hili Juni 30, 2024.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha pia ametangaza kuunda kamati maalum ya rufaa itakayosimamia safari mbalimbali za wagonjwa watakaobainika kuhitaji matibabu ya ziada kwenye hospitali za kanda na Taasisi za afya akitangaza pia kuufahamisha umma kuhusu utaratibu mpya wa kuhudumia Wazee, watoto na akina mama wajawazito ili kuwaepusha na kukaa muda mrefu kwenye misururu.

No comments