AGA KHAN YATOA MSAADA WA CHUMBA BARIDI CHA KUHIFADHIA CHANJO NA DAWA MKOANI ARUSHA.
AGA KHAN YATOA MSAADA WA CHUMBA BARIDI CHA KUHIFADHIA CHANJO NA DAWA MKOANI ARUSHA.
Taasisi ya Huduma za afya Aga Khan nchini Tanzania imetoa Chumba baridi maalum chenye thamani ya Milioni 56 kwa Mkoa wa Arusha maalum kwaajili ya kuhifadhia dawa na Chanjo kwenye Halmashauri ya wilaya ya Karatu.
Chumba baridi hicho kimekabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda na Bi. Theresia Mhere, Meneja miradi wa Aga Khan na kisha Kumkabidhi Ndugu Juma Hokororo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu tayari kutumika kwenye Wilaya hiyo muhimu kwa Utalii na uchumi.
Wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika kwenye viwanja vya Sheikh Amri Abeid kunakoendelea Kambi maalum ya matibabu ya kibingwa, Bi.Theresia amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa Aga Khan itaendelea kushirikiana na Mkoa katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wakazi wa Arusha.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha naye ameishukuru Taasisi hiyo ya afya kwa msaada huo na kusema kuwa wamekubaliana mashine hiyo kwenda wilayani Karatu ili kutoa hakikisho la usalama wa dawa na chanjo kwa watalii wanaotumia Wilaya hiyo kama lango la kuingilia kwenye hifadhi zilizopo kwenye ukanda huu.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu Mhe. Juma Hokororo amemshukuru Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa jitihada zao katika kuboresha sekta ya afya Mkoani hapa na kuahidi kusimamia matumizi sahihi ya chumba hicho kwa manufaa ya wananchi wa Mkoa wa Arusha.
No comments