TCRA YATOA AHUENI KWA BLOGA, WANAMITANDAO
Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa nafuu ya kutolipa ada ya mwaka mmoja kwa waandishi wa habari wanaoanzisha mitandao ya habari kwa mara ya kwanza ambapo imeelezwa kuwa watajulikana kama 'Amateur'.
Nafuu hiyo, imetengazwa na Meneja wa Huduma za Utangazaji wa TCRA,Mhandisi Andrew Kisaka alipokuwa akiwasilisha matokeo na utekelezaji wa mapendekezo yatokayo na utafiti wa huduma za utangazaji nchini katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji Februari 12, 2026 jijini Dodoma.
Mhandisi Kisaka amesema kuwa wametoa nafuu hiyo ili kuwapa muda waandishi wa habari wa kujifunza na kupata uzoefu wa uendeshaji wa mitandao.
Awali anayetaka kuanzisha mtandao wa habari alitakiwa alipe ada ya maombi Sh. 50,000 na ada ya leseni sh. 500,000 kwa mwaka.
Hatua hiyo, imepokelewa kwa furaha na wamiliki wa mitandao waliohudhuria mkutano huo ambao baada Mhandisi Kisaka kutangaza walipiga makofi.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo ni wanachama wa Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN), Jumuiya ya Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA), Jukwaa la wahariri Tanzania (TEF), MOAT, NIBA, Wakongwe RTD, Baraza la habari Tanzania (MCT), MISA Tanzania na EACO.
No comments