Serikali ya Rwanda yaanza mchakato wa kuandaa Sheria ya kupiga marufuku matumizi ya Mitandao ya kijamii kwa Watoto Chini ya miaka 16

Serikali ya Rwanda imeanza mchakato wa kuandaa Sheria itakayoweza kupiga marufuku matumizi ya Mitandao ya kijamii kwa Watoto walio chini ya umri wa miaka 16, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ulinzi wa Watoto Mtandaoni.

Kwa mujibu wa taarifa za Serikali, taasisi mbalimbali nchini humo zinashirikiana kuandaa rasimu ya sheria hiyo, ambayo inalenga kuwalinda Watoto dhidi ya maudhui hatarishi, unyanyasaji wa Mtandaoni pamoja na vitendo vya unyonyaji vinavyoweza kujitokeza kupitia majukwaa ya kidijitali.

Hatua hiyo inakuja wakati matumizi ya intaneti na Mitandao ya kijamii yakiongezeka kwa kasi nchini Rwanda, hali inayoongeza hatari kwa Watoto kukumbana na changamoto za usalama wa mtandaoni.

Hata hivyo, maelezo ya kina kuhusu sheria hiyo bado yanaendelea kujadiliwa, ikiwemo namna ya kuthibitisha umri wa watumiaji na wajibu wa kampuni za mitandao ya kijamii katika kuhakikisha Sheria hiyo inazingatiwa.

Iwapo itapitishwa, Sheria hiyo itaifanya Rwanda kuwa miongoni mwa nchi chache zinazochukua hatua kali kudhibiti matumizi ya Mitandao ya kijamii kwa Watoto, huku mjadala ukiendelea kuhusu uwiano kati ya ulinzi wa Watoto na haki zao za kidijitali.


#KitengeUpdates

No comments