WATOTO MAKAO WAJENGWE KISAIKOLOJIA: WAZIRI DKT. GWAJIMA

News Images

Serikali imewataka wamiliki wa makao ya kulea watoto kuwaandaa kisaikolojia watoto kupitia huduma zinazotolewa na mipango ya kuwaondoa makaoni.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa maadhimisho ya Miaka 20 ya makao ya watoto yatima wasiojiweza Kijiji cha Matumaini Jijini Dodoma Agosti 17, 2022.

Waziri Dkt Gwajima amesema mchakato huo usipofanyika ipasavyo husababisha watoto kuona Makao ni nyumbani kwao na sehemu ya kudumu, hivyo kulelewa hadi utu uzima na mara nyingi wakitoka makaoni hushindwa kujitegemea, kuishi katika familia zao au kutengamanishwa katika jamii.

"Kupitia siku hii muhimu, nawaagiza wamiliki na waendeshaji wa Makao nchini kuhakikisha kila mtoto anayepokelewa makaoni anaandaliwa mpango wa huduma unaojumuisha mpango wa kutoka Makaoni na taarifa zote zihifadhiwe katika jalada la mtoto" amesema Waziri Dkt. Gwajima.

Amewaagiza pia Maafisa Ustawi wa Jamii kote nchini kuhakikisha agizo hili linatekelezwa katika maeneo yao na Msajili wa Makao, Kamishna wa Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI wafanye ufuatiliaji ipasavyo.

Amesema idadi ya Watoto 145 wanaolelewa katika makao hayo ni sehemu ya Watoto 24,454 wanaolelewa katika makazi 324 yaliyosajiliwa nchini yakiwemo makao mawili ya Serikali ya Kurasini Dar es Salaam na Kikombo Dodoma.

"Hata hivyo malezi ya watoto makaoni ni suluhisho la mwisho wakati sababu zilizochangia zikiwa zinafanyiwa kazi" alisema Waziri Gwajima.

Aidha, Waziri Dkt Gwajima ameahidi kushirikiana na Mamlaka zinazohusika kusaidia ufumbuzi wa changamoto ya utozwaji kodi katika miradi iliyobuniwa ambayo inaathiri utumiaji wa mapato katika kukidhi mahitaji mbalimbali ya watoto wanaolelewa makaoni hapo.

Akisoma risala ya makao hayo, msimamizi wa Utawala katika Kijiji cha Matumaini Baltazar Sungi amesema makao hayo yaliyoanzishwa mwaka 2022 yanatumia mfumo wa familia kwa wanakaya kujitolea kuwatunza

watoto hao.

"Hivi sasa watoto wanaohudumiwa hapa ni 145, 62 wavulana na 85 ni wasichana kutoka sehemu mbalimbali Tanzania na walezi 26 wa kujitolea" alisema Bartazar.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Mhashamu Beatus Kinyaiya ameiomba Serikali makao hayo kutambuliwa kama watoa huduma za hisani ili wapunguziwe baadhi ya kodi.

Kwa upande wa mmoja wa wanufaika waliolelewa katika makao hayo pamoja na mlezi wake Elizabeth Gamaka wameshukuru kwa uwepo makao hayo na kuwaasa wazazi wanaotelekeza watoto kuacha tabia hiyo.

Maadhimisho hayo wameenda sambamba na harambee ya ujenzi wa baadhi ya Majengo kwenye Kijiji hicho ambapo Serikali kupitia Wizara imechangia jumps ya shilingi Milioni tano.

MWISHO

Tanzania Census 2022

No comments