JIJI LA ARUSHA LATOA MSAADA WA KISHERIA KWA JAMII.
Na.Vero Ignatus,Arusha
Katika kuadhimisha wiki ya sheria iliyoandaliwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha na kuwajumuisha wadau wa sheria ikiwemo TAMWA, Inherit Your Right,vimeweka juhudi katika kuhakikisha kuwa Jamii inapata uelewa wa kutosha juu ya msaada wa kisheria,ikiwemo Kupinga Ukatili na unyanyasaji wa Kijinsia kwa wanawake , watoto na Jamii kwa ujumla.
Akizungumza Mwanasheria kutoka Jiji la Arusha Marry Mwita amesema kuwa Ukatili mwingi unachangiwa kwa wazazi wengi kusahau suala la malezi na kujikita zaidi katika kutafuta pesa jambo ambalo linachangia ongezeko la matukio ya ukatili wa kijinsia.
Mwita alisema kuwa tatizo la ukatili wa kijinsia kwenye jamii linatokana na wazazi kutumia muda wao mwingi katika kujitafutia kipato na kusahau wajibu wao kwa kuwa karibu na watoto ili kuwapa malezi bora na kujua changamoto zinazowakabili watoto hao.
Akizungumza wakiwemo Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA) pamoja na Shirika lisilo la kiserikali la Inherit Your Right,
Amewashauri wazazi kutumia muda mwingi kuwasikiliza watoto kwani wengi wanapitia changamoto nyingi lakini kwa kuwa wazazi hawapo karibu nao inapelekea watoto kuendelea kuumia na kuathirika zaidi hata kuwasababishia madhara makubwa yakiwemo ubakaji, ulawiti na hata kushababishiwa vifo
Akizungumzia ukatili ndani ya ndoa, Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Inherit Your Right Wakili, Winnefrida Manyanga amesema kwa kiwango kikubwa ukatili ndani ya ndoa ni matokeo ya kuvumilia madhila wanayokutana nayo kwa muda mrefu bila kutafuta msaada wa kisheria jambo ambalo hupelekea madhara makubwa baadaye yakiwemo mauaji.
“Unaweza kukuta mama anapigwa sana na mume wake, lakini ukimuuliza sababu ya yeye kuvumilia bila kutafuta haki yake kisheria anasema anavumilia kwa sababu ya watoto wake, au anasema anavulimia kwa sababu ya mali zake alizotafuta kwa jasho lake, unajiuliza kwani akiondoka pale akaishi sehemu nyingine kwa amani hawezi kuwalea watoto wake na akapewa haki kwa maana ya mali alizotafuta? Aliuliza Wakili Manyanga na kuongeza.
“Yote haya ni kwa sababu baadhi ya wanajamii hawajui kuwa kuna sheria zinazomlinda kila mtu, ukiona unaishi kwa mateso ya ukatili hupaswi kuvumilia kisa unalea watoto, wala hupaswi kuvumilia kisa utaacha mali zako, sheria ipo…..watoto wako utawalea kwa amani na mali yako hutaipoteza, hivyo ni wakati sasa wa kuacha kuvumilia madhila madogo madogo lakini mwisho wa siku yanaweza kuleta madhara makubwa” Alisema.
Mwakilishi wa Ashura Mohammed amesema ,TAMWA kwa kushirikiana na vyombo vya dola imeendelea kuibua matukio ya ukatili wa kijinsia katika jamii na kuishauri jamii kutumia vyombo vinavyotambulika kisheria kuripoti kesi zote zinazohusiana na ukatili wa kijinsia badala ya kumalizana majumbani kama ambavyo hufanyika kwenye baadhi ya jamii kwani kitendo hicho kinaminya haki ya muathirika wa vitendo hivyo.
“Ukatili wa kijinsia unaathiri zaidi watoto, hivyo wazazi kabla ya kufanya maamuzi yoyote ni vyema mkaangalia hatma ya watoto wenu, hakuna mtoto anayependa kuona wazazi wakigombana, wakipigana au wakitengana, hii ina athari sana kwenye makuzi yao na hata kuua ndoto zao” Alisema Ashura
No comments