RAS ARUSHA ASISITIZA MOTISHA KWA WATUMISHI WA UMMA


•Ataka motisha chanya na sio vyeti vya pongezi, "vyeti havina tija kwa watumishi, ukitaka kumtumia punda mpe chakula apate nguvu. 
 

"Jambo lingine ni motisha kwa watumishi, punda ukitaka kumtumia vizuri lazima umlishe apate nguvu, ngombe ukitaka kumkamua atoe maziwa mengi lazima umlishe vizuri na kumpa maji mengi, hawa watumishi ukitaka wafanye kazi vizuri kwa waledi na maarifa ya hali ya juu, wakiwa na afya nzuri ya akili na mwili lazima kutoa motisha chanya"

Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Dkt.Toba Alnason Nguvila amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu kuwapa motisha chanya watumishi wake, ili waweze kuipenda kazi yao na kuweza kufanya kazi kwa welezi na maarifa yote.

Amesema hayo wakati wa kikao kazi cha kwanza na watumishi wa Halmashauri ya Karatu tangu alipoteuliwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa shule ya sekondari Karatu.

Dkt. Nguvila pia amekemea tabia ya Wakurugenzi kuwapa vyeti watumishi wanaofanya vizuri na kufafanua kuwa,  watumishi hawali vyeti akitaka zawadi hizo ziboreshwe, wapewe pesa na wakati mwingine hata kuwapeleka kwenye mbuga za wanyama kutalii.

"Mkurugenzi mtumishi hali cheti, mpeni kitita cha pesa, wakati mwingine mnayo maeneo mengi mpeni kiwanja mtumishi aliyefanya vizuri, zawadi ambayo itakua historia hata kwa kizazi chake. Karatu ni kitovu cha utalii, waandalie safari ya kwenda mbuga za wanyama, wakaondoe stress, Mkurugenzi watumishi hawa wanahitaji kupewa motisha ili waweze kukusaidia". Amesistiza Dkt.Nguvila.

Hata hivyo amesisitiza, Wakurugenzi  kuwajali sana watumishi wa chini, masekretari, madereva, wahudumu na watunza kumbukumbu na kuhakikisha wanashiriki kwenye mikutano yao ya kitaaluma ya mwaka,  kwa kuwawezesha usafiri na posho za kushiriki vikao hivyo ambavyo hufanyika mara moja kwa mwaka.

No comments